Dunia Ya Pili - 02 
Butwaa nililopigwa nalo halikuwa na mfano! Taa nyekundu iliwaka kichwani mwangu, nilihisi kitu kibaya juu yangu ingawa sikutaka kujihakikishia moja kwa moja.
“Meddy mwanetu yupo wapi?”
Nilijikuta nimeuliza swali lile pasipo mimi kutegemea.
“Yupo.”
Alijibu ingawa jibu lake lilioneshwa wazi kabisa halikutoka moyoni bali lilitoka kinywani tu.
“Yupo wapi?”
Nilimhoji mara ya pili wakati huo nikimtizama Amina, nilimwona akimtizama kaka yake usoni.
“Ameenda chumba cha joto.”
Alijibu Meddy nikamuona Amina akishusha pumzi.
Sikuridhika na jibu lile ingawa nisingeweza kumpinga, jibu la Meddy sikuridhika nalo moja kwa moja.
Siku ya pili majira ya mchana baadhi ya ndugu waliondoka hospitalini nikabaki na Medy pamoja na wifi yangu Amina.
“Shangazi kaja?”
Nilimuuliza Meddy siku hiyo mchana.
“Alikuja leo lakini aliondoka hatujui kama yupo bado au ameenda nyumbani.”
Alijibu Meddy.
Nikastaajabu.
“Shangazi kwanini hataki kuwa karibu na mimi?”
Nilijiuliza.
“Kwahiyo haujui alipo?”
Niliuliza.
“Sijajua sababu hakuaga ila nahisi atakuwa ameenda nyumbani kwake.”
Alijibu Meddy.
Nikabaki na tafakari nzito kichwani mwangu.
Siku hiyo ndiyo siku niliyogeuka kero wodini nikimdai mwanangu.
Meddy alijaribu kunituliza lakini nilimtolea nje, nikawa mkali kama nge!, niliwaka siyo kitoto.
Kuona hivyo Meddy aliamua kumuita Amina nae akaja kujaribu kunituliza lakini sikuwaelewa.
Baadae nikataka kupiga mayowe ili wauguzi waje niwarushie matusi ya nguoni, nilipanga kufanya hivyo ili nijue hatima ya mwanangu.
“Tulia wifi ya dunia mengi kuna kupata na kukosa hivyo kaza roho tuliza moyo na utafakari maisha yako.”
Aliongea Amina nikatulia ghafla kama sanamu huku nikimtizama usoni.
“Sijakuelewa.”
Niliongea huku moyo ukianza kupiga puta.
Amina alinisogelea na kisha kwa upole kabisa aliniambia kuwa mwanangu sipo nae kwani alifariki muda mfupi tu baada ya upasuaji kukamilika,
haifahamiki nini kilimuua hata madaktari walipompima hawakubaini sababu iliyomuua mwanangu hivyo bado yupo chumba cha kuhifadhia maiti,
wanandugu walikuwa wanafanya vikao uko nje kwaajili ya taratibu za mazishi.
Meddy aliangua kilio!
Moyo ulilipuka sambamba na uchungu mkubwa wa tumbo pumzi ikanibana nikashindwa kufanya chochote!
Nguvu zikaniishia nikahisi kiza mbele yangu.
Ghafla nilizinduka mithili ya mtu alietokea kwenye usingizi mzito! Nilizinduka nikajikuta kati kati ya msitu mmoja mnene tena nikiwa peke yangu!
Nilistaajabu nikakurupuka kama mwehu huku nikihema kwa nguvu sababu ya kiroho cha uoga.
Nilisimama na kutizama huku na kule, nikashituka zaidi pale nilipobaini kuwa mazigira yale yalikuwa mageni kabisa machoni mwangu.
Siyo hivyo tu bali taswira ya eneo lile ilitisha mwonekano wake haukuwa wa kawaida.
Kwanza hakukuwa na jua! Ingawa kulikuwa na mwanga mweupe ufananao na wa jua.
Miti yake ilikuwa na mwonekano wa kipekee mwonekano ambao sidhani kwa duniani kama kuna sehemu yenye miti ya aina hiyo!
Kingine nilichobaini ni kwamba eneo lile lililokuwa na milima, milima yake ilikuwa ikijibadilisha mwonekano mithili picha za animation!
Niliogopa sana, nikatamani kukimbia ingawaje sikuona pa kukimbilia!
Pumzi ikajaa kifuani nikatizama kushoto na kulia nikiwa nimetandwa na hofu kuu moyoni.
Nikashusha pumzi nzito.
“Fuuuu”.
Mara nilisikia sauti ya mtoto mchanga akilia umbali fulani kutoka pale nilipokuwepo, ghafla nilikumbuka kuwa saa chache zilizopita nilijifungua
mtoto nilivyojitizama sikumuona!
Papo hapo akili ikaniambia kuwa huyo ndiye mwanangu.
Sikukawia kutimua mbio! Kuifuata sauti hiyo itokeapo.
Cha ajabu sasa kila nilivyozidi kwenda mbele sauti nayo ilizidi kusikika mbele zaidi, nami nikazidisha mbio mara dufu, ghafla mtoto aliacha kulia!
Nikaduwaa!
“Huyu mtoto yuko wapi?”
Nilijiuliza saa hiyo nikiwa nimesimama nikisikiliza huku na kule.
“Ng’aa… ng’aa… ng’aa!”
Mara nikasikia mtoto akilia nyuma nilikotokea! Duuh, nikapagawa!
Nikarudi mbio, huwezi amini nilikuwa nikitimua mbio kali huku nikiruka manyasi kama mwehu vile, nilikimbia nikiifuata sauti hiyo anakolia
huyo mtoto cha ajabu sikufika zaidi ya kuifuata sauti hiyo.
Mwisho mtoto alisitisha kilio kwa mara ya pili nami nikasitisha mbio zangu!
Nilishusha pumzi, nikabaki nikihema kama mwana riadha alietoka shindanoni.
Nilisikiliza huku na kule mara nikasikia tena mtoto akilia.
“Ng’aa! Ng’aa! Ng’aa.”
Safari hii sauti hiyo ilisikika jirani zaidi, nikatoka mbio!
Niliongeza spidi, nilikimbia kwa kasi ya kushangaza mpaka nikaenda kuingia kati kati ya msitu mnene wenye miti mirefu, mikubwa na yenye matawi mengi
yaliyojistawisha vyema kabisa na majani.
Nilipoingia mle mtoto aliacha kulia!.
Nilichukia, nikasimama na kutukana matusi ya nguoni huku uso wangu ukiwa umefura kwa hasira.
“Ng’aa! Ng’aa! Ng’aa!”
Mara nilisikia mtoto akilia juu ya mti!
Nilipigwa na butwaa!
Haraka nilinyanyua uso wangu nikatizama juu ya mti.
Butwaa nililopigwa nalo halikuwa na mfano! Muda huo huo nilihisi sehemu zangu za siri zikiloa kwa jasho.
Nilitetemeka!
Nilitamani nitimue mbio kali lakini nilihisi miguu imekosa nguvu.
Juu ya mti ule mkubwa uliokuwa kati kati ya ule msitu alikuwepo nyoka mkubwa mnoo aina ya chatu aliekuwa kajiviringisha kwenye matawi ya kati kati ya ule mti.
Nyoka huyu ndiye aliekuwa akilia sauti ile ya mtoto mchanga, na kila alivyokuwa akilia mdomo wake ulikuwa ukitoa michili myembamba ya damu pembezoni.
Nilishindwa kuelewa wala kuamini kuwa kile nilichokuwa nikikitizama kwa muda ule ilikuwa ni kweli au ndoto ama zingaombwe fulani la kutisha.
“Nini hiki?”
Nilijiuliza!
Mara lile joka liligeuza kichwa chake taratibu likanitizama huku chini, hakika macho ya joka lile yalitisha mara tatu ya macho ya mbwa yatishavyo
pindi amulikwapo na tochi akiwa gizani.
“Hahahaa! Usiogopee! Usiogopee! Usiogopee! Karibu katika ulimwengu pendwa! Ulimwengu ambao agano lake liliwekwa na mababu wa kale,
hivyo tunakukaribisha Leylah kuwa mmoja kati ya wanafamilia pendwa katika mji huu, mji mtukufu, mji teule na wenye kila aina ya neema.”
Nilistaajabu kuona nyoka anaongea, mshangao niliotokwa nao saa ile ulikuwa ni mshangao mkubwa mara tano zaidi ya ule wa kawaida.
“Karibu sana!”
Liliongea joka hilo.
“Kwani wewe nani?”
Nilijikaza nikatoa sauti kuuliza swali hilo huku nikiwa nimetawaliwa na hofu kuu moyoni.
“Hahaha mimi ni kiumbe mkubwa na mwenye nguvu kubwa sana katika ulimwengu huu!”
Joka lilijibu huku likichezesha mwili kwenye matawi, nayo matawi yakatikisika, nami nikahisi miguu ikicheza chini.
Nilishusha pumzi nikameza mate ya uoga, hakika yule kiumbe alikuwa anatisha siyo siri.
“Karibu sana!”
“Mimi sipo tayari kuishi na nyinyi.”
Nilipayuka!
“Hahaha… Sawa nitakuonesha mwanao alipo, ukiweza kumchukua basi utaweza kujitoa katika agano lililowekwa na mababu zenu kuhusu ulimwengu huu na familia yenu…
Ukishindwa basi habari yako itaishia huku!”
Lilisema joka lile.
Ghafla mazingira yalibadilika! Kilikuwa ni kitendo cha kufumba na kufumbua tu, ile miti sikuiona wala lile joka badala yake niliona msitu mwepesi na wa kawaida.
Muda huo huo nilianza tena kusikia sauti ya mtoto akilia.
Nilianza tena kuifuata sauti hiyo niliifuata mpaka nikafika sehemu palipokuwa makutaniko ya mito miwili,
ilikuwa ni sehemu yalipokutania maji ya mito miwili tofauti, ilikuwa ni sehemu pana na yenye mawe ya kutisha, maji yaligongana kwa fujo na
kusababisha mawimbi makubwa ya maji hata yakatoa moshi utafikiri yanachemshwa!
Nilistaajabu!
Pembeni ya eneo hilo ndani ya mto kuna joka kubwa lilikuwa limejiviringisha na kutengeneza duara kubwa kwenye ukuta wa kutaniko lile la mto
kisha kuna mtoto alikuwa kakaa juu ya lile joka kisha kabanwa na mkia huku mtoto huyo akilia mfululizo.
“Yesuuuuuuu!!!…”
Nilipiga ukunga mkubwa, ghafla nikakurupuka kitani nikakuta namwagiwa maji huku wauguzi wakiwa wametingwa kwa kiasi cha kutisha! Amina alikuwa pembeni akilia tu!
Nilishangaa!
Unaweza pia kusoma: