Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Dunia Ya Pili - 04

Nilishangaa kwa kile kilichokuwa kinaendelea, sikujua nafungwa kamba kwa sababu gani na wakati nikiwa bado naendelea kushangaa niliona wanaendelea kubishana pale.
“Ana mapepo jamani ngoja tumuombee.”
Aliongea wifi Amina.
“Hapana!”
Shangazi alipinga.
“Huyu kachanganyikiwa tu hana mapepo wala nini tumrudishe nyumbani akapumzike.”
Alisema shangazi.
“Ana pepo huyu huoni alikimbia pale wakati nilipoanza kuomba?”
Aliongea Amina, nikatumbua macho.
Nilishangaa kusikia nilikimbia wakati mimi sikukimbia.
“Ndiyo maana nimekwambia alichanganyikiwa mbona siyo mwelewa wewe?”
Shangazi alianza kuwaka, ikabidi Amina awe mpole tu.
Basi palepale ilipigwa simu boda ikaja kunichukua ikanipeleka moja kwa moja mpaka nyumbani.

Huko nilikuta umati mkubwa wa watu wakilia mno!
Wakiwemo wakwe zangu na ndugu wengine wengi sana, akili ikaniambia huo ulikuwa ni msiba wa mwanangu, mwanangu ambae hata kumuona tu sikumuona!
Yalinijia mawazo ya ajabu yaliyojawa na uchungu mkali, nikajikuta napiga yowe kali, ghafla nikajikuta ndani ya msitu mnene nikiwa natizamana ana kwa ana na yule kiumbe atishae kupita kawaida.
“Umeanza kuharibu utaratibu siyo?”
Yule kiumbe aliniuliza huku macho yake yakiwa mekundu kama makaa ya moto.
Sikujibu nilitulia huku nikitetemeka mwili mzima kwa hofu kubwa iliyojijenga moyoni.
“Hutakiwi kulia, kwani ukilia utamfata mwanao halafu mwambie huyo wifi yako akiona hawezi kuhudhuria msiba huo bila kuomba omba aondoke hapo haraka iwezekanavyo.”
Alipomaliza kusema hayo yule kiumbe nilizinduka nikajikuta nipo kitandani nikiwa napepewa na kitenge, siyo siri kwa kile kilichokuwa kinaendelea juu yangu waliokuwepo walijua nazimia kwasababu ya kumpoteza mwanangu lakini kumbe haikuwa hivyo bali kulikuwa na siri nzito mno nyuma ya pazia.

“Pole.”
Ilikuwa ni pole kutoka kwa wifi yangu Amina.
“Asante wifi.”
Nilijibu huku nikimtizama usoni, kuna muda nilimuonea huruma kwa kile kilichokuwa kinaendelea juu yake bile yeye kujua, nilielewa fika wale viumbe kutoka Dunia ya pili ni lazima wangemtafutia mbinu ya kumpoteza sababu ya ukaribu wake na mimi.
Sauti yangu niliyoitoa kumjibu wifi iliwaliza wote waliokuwa pale walilia na mengi sana isipokuwa mimi tu, nilishindwa kulia sababu ya mambo yaliyokuwa yanaendelea juu yangu.
Kweli mpaka msiba wangu unaisha sikutoa machozi tena tangu onyo kutoka Dunia ya pili hadi baadhi ya watu walinishanga na kujiuliza kwanini sikulia?
Kwamba sikuwa na uchungu wa kumpoteza mwanangu?
Hayo yote yakawa siri yangu mpaka msiba uliisha watu wakatawanyika hatimaye kwa mara nyingine tukabaki mimi na mume wangu Meddy maisha yakaanza upya mara nyingine tena.
Wiki mbili za mwanzo tuliishi kwa hudhuni lakini ulipokata mwezi tulianza kusahau na kuchukulia kama ni hali ya kawaida kwa kila mwanadamu.
Shangazi alianza kujiweka upya karibu na mimi ingawa mimi bado nilikuwa na kinyongo nae kwasababu ya yeye kunitenga pindi nimeolewa na Meddy.

Siku moja mida ya mchana, siku hii Meddy alikuwa ameondoka kwenda mihangaikoni, sasa mchana ule nilipata wazo la kufua ikabidi nikusanye nguo zote nikazipeleka nje kwaajili ya kuzifua, lakini kabla ya kufua kuna akili ilinijia ikanitaka nikague nguo zote kama zilikuwepo ili nianze rasmi kufua.
Baada ya ukaguzi niligundua khanga moja haipo.
“Hii nguo ipo wapi?”
Nilijiuliza saa hiyo nikirudi ndani kuitafuta.
Kituo cha kwanza nilifikia kwenye tranka sababu baadhi ya nguo za muhimu sana nilikuwa nahifadhi kwenye tranka, nilifikia na kukifungua nikashangaa hiyo nguo naikuta juu mwanzoni kabisa tena ikiwa imerundikwa tu bila kukunjwa vizuri nilishangaa sababu haikuwa desturi yangu kuweka nguo kwenye tranka bila kuikunja vizuri, hata hivyo sikuwaza sana niliiamua kuichukua tu.
Mara nashituka kugundua nguo hio ni nzito kana kwamba imefungwa kitu.
Niliitoa kwenye tranka kisha nikalifunga vyema ndipo nikaikunjulua na kuikagua, kweli nikakuta imefungwa kitu mithili ya jiwe, haraka nikafungua ili nione nini hicho kilichofungwa hapo.
Nakutana na mfuko mweusi wa nailoni, nao niliufunga haraka ghafla nikaganda kama sanamu.

Jiwe kubwa lenye rangi ya dhahabu inayong’aa sana nilikutana nalo ndani ya mfuko ule wa nailoni mweusi, nilitulia kwanza nikilitizama jiwe lile.
“Baba amenituma nikupe huu mzigo, amesema ukifika kwenu upeleke benki utapata hela nyingi sana, basi utaanzia hapo sawa?”
Nilikumbuka maneno hayo nikaelewa nini maana ya lile jiwe, hakika moyoni niliingia na robo ya furaha hasa nilipokumbuka hali ya maisha ilivyokuwa ngumu wakati ule nilijikuta nikitabasamu kwa mbali.
Lile jiwe nililihifadhi vizuri chini ya nguo kwenye tranka kisha nikalifunga vyema nikarudi nje kuendelea na harakati za ufuaji.
Nilifua mpaka namaliza, mishale ya alasili, mume wangu alirudi akiwa kachoka sana.
“Waaooo!”
Nilimkimbilia na kumkumbatia, nikambusu mabusu kadhaa kisha nilimpa pole na kazi, yote hayo nilimfariji ili ajiskie amani moyoni.
Nilimpokea kimzigo alichokuwa nacho mikononi kisha nilitangulia ndani nae akanifata.
“Nilikumiss mke wangu.”
Aliongea Meddy wakati huo akipunguza nguo zake.
“Hunishindi mimi mume wangu, hivi nimefua hadi namemaliza huku mara kwa mara nikitizama njia nikihisi labda nitakuona lakini wapi. Hee wewe hata huruma huna?”
Niliongea saa hiyo nikiwasha moto kwenye jiko la mkaa kwa kuupuliza na mfuniko wa kindoo.
“Dah! Acha bwana kazini hata raha nikawa sina ujue.”
“Uwongo huo!”
“Dah! We acha tu.”
“Lakini pole,nashukuru sana umerudi salama.”
“Asante sana nami nashukuru pia kukukuta salama na wewe mke wangu.”

Niliwasha jiko nikatenga maji yake ya kuoga wakati huo yeye akiwa kapanda kitandani, nikamfuata.
Niliendelea kumfariji kwa maneno matamu huku nikimpeti peti hatimae kitanda hakikuzaa haramu.
Baadae maji yalichemka tulioga kwa pamoja, baadae niliingia jikoni nikapika tukala.
Baada ya chakula tuliendelea kuongea maongezi ya kindoa mpaka siku iliisha hatimaye usiku uliwadia, muda wa kulala ukawasili kwa pamoja tulipanda kitandani tayari kwa safari ya kuusaka usingizi.
Tuliongea machache tu mara nilihisi usingizi mzito ukinijia.

Nikarazimisha kufumbua macho kwani sikutaka kusinzia muda ule, kufumbua macho nilijikuta niko ndani ya jumba moja kubwa na la kifahari mno.
Mbele yangu alikaa mtu mwenye sura tatanishi, aliejivika mavazi makubwa ya kifalme akiwa kaketi kwenye kiti kilichotengenezwa kwa madini ya dhahabu.
Kupitia madirishani niliweza kuona kundi kubwa la mizuka walioshikilia silaha zao wakiendelea kuimarisha ulinzi nje ya jengo lile ambalo bila shaka nilihisi ni ngome.
“Karibu!”
Yule kiumbe alinikaribisha.
Nasema kiumbe kwa sababu hakuwa binadamu kama mimi.
“Najua ulifurahi sana kuona uwepo wa dhahabu kubwa ndani ya nyumba yako si ndiyo hivyo?”
Aliuliza yule kiumbe.
“Ndiyo.”
Nilijibu.
“Safi sana! Sasa wewe kwako umasikini basi, maana yake unaupungia mkono kuanzia sasa.”
Aliongea yule kiumbe huku akinyanyuka kitini kwake.
Aliondoka hatimae alirudi na chungu kidogo cheusi tii, akanisogezea kile chungu akaniambia nisonde kidole ndani.
Mwanzoni nilisita lakini yule kiumbe alinishawishi kwa maneno mazuri hadi nikafanya vile!
Ghafla nilishituka usingizini nikakurupuka kama mwehu baada ya kusikia mume wangu Meddy amepiga yowe kali huku akirusha rusha miguu na mikono huku na kule hata akanipiga na mimi.
Taa ilikuwa imezimwa, nilinyanyuka kwa kasi mpaka usawa ilipo swichi nilipapasa nikaiona nikaibonyeza, taap!
Taa ikawaka mwanga mweupe ukasambaa chumba kizima.
La haula! Nilipigwa na butwaa kuona Meddy akiwa na jeraha kubwa la kisu tumboni, damu zikimwagika kama maji huku kisu kikiwa chini.
Harufu kali ya damu iliyokuwa imeenea chumba kizima ilifanya nijiangalie…
Tobaa!
Nilitamani kupiga yowe kubwa baada ya kuona mkono wangu wa kulia ukiwa na damu nyingi huku zingine zikiwa zimenirukia kifuani na shehemu mbalimbali za mwili.
Nilivurugwa!
Nikapagawa…
Nikiwa bado katika hali ile ya sintofahamu mara nilisikia kundi la watu wakija huku wakiendelea kuitana, wakati huohuo nilimsikia baba mkwe akifungua mlango kwa nguvu kwenye nyumba wanayolala, huku akiuliza kwa sauti ya juu…
“Kuna niniiiiiiiii?”

Sehemu 3 Sehemu 5
0
0