Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Dunia Ya Pili - 21

Baada ya kwisha kuliegesha gari tulishuka na kuingia ndani ya ngome hiyo kubwa na yenye hadhi yake.
Humo ndani walikuwepo watu wachache ambapo kwa zamu kila mmoja alikwenda kuonana na Lucifer aliekuwa kaketi katika kiti chake cha kifalme.
Huyu kiumbe hajawahi kuwa na sura moja, kila nilipomwona alikuwa na sura tofauti na niliyomwona nayo awali, na leo hii alikuwa kajivika sura ya dubu kisha macho na mdomo alifanana kwa kila kitu na paka mweusi, alitishia kiumbe yule si utani.
Ilifika zamu yangu baada ya Sam, nilikwenda.
Nilifika pale na kutoa heshima yangu kisha nilipewa bahasha iliyotuna sikujua ndani ilikuwa na kitu gani.
“Kuna mtu anaitwa Abdalah Kizau huyu mtu unatakiwa kumuondoa duniani leo usiku kabla hakujakucha kesho…
Huyu mtu katusaliti mbaya zaidi kaenda kutoa ushuhuda wa siri zetu kanisani baada ya kujifanya ameokoka.”

Moyo ulipiga puu! Kuua tena? Dah!
“Usiogope ni rahisi sana kumpata, atakuwa Miami leo usiku akiwa na mwanamke anaitwa Angel Devil ameingia kwenye mtego wetu pasipo yeye kujua nenda kamuue huyo Angel Devil baada ya kazi atapotea na kurudi zake kuzimu kwani alikwenda duniani kwa kazi hiyo tu na sasa inakwenda kukamilika.”
Aliweka kituo kiumbe yule.
Nikashusha pumzi.
“Nimekupatia millioni hamsini kama kianzio, baada ya kazi utapewa milioni hamsini zingine kama pongezi.”
Nilivyosikia neno milioni hamsini tu, nilipagawa kama mwehu vile nilihisi akili inawasha kwenda kuifanya kazi hiyo mara moja nifate kitita kilichosalia hakika nilianza kuona pesa kwangu sasa ni uchafu!
Hata cha kufanyia tena sikuona.
“Nenda zako kajiandae na kazi.”

Aliniruhusu nami nikaondoka, Sam hakuwepo tena hivyo nilianza kuondoka ile nafika mlangoni kufumba na kufumbua nikajikuta nanyanyuka kitandani huku haja ndogo ikiwa imenibana nusu ya kujikojolea.
Hee ilibidi niamke upesi na kukimbilia chooni huko nilimwanga maji mengi sana hiyo ni sababu ya bia nilizokunywa kabla ya kulala.
Baada ya kumaliza haja yangu nilirudi chumbani huko nikakutana na bahasha nyeupe ikiwa kitandani kwa kuwa nilikuwa naelewa kila kitu hata sikuishtuka nilichokifanya ni kuifungua bila hata papara yoyote.
Nikatabasamu baada ya bahasha kufunguka nilikutana na maburungutu matano ya maana yakiwa yamebanwa vyema na mpira zilikuwa ni pesa mpya kabisa ambazo hazijawahi hata kuguswa tangu zichapwe!
Halafu pesa hizo ziliambatishwa na picha ya huyo Abdalah Kizau.
Duh!
Nikaifunga tena bahasha hiyo, na kwa kuwa nilioga kabla ya kulala sikuona tena ulazima wa kuoga muda ule nilichokifanya ni kuvaa tu nguo zangu.
Ilikuwa yapata saa kumi na dakika hamsini alasili, zikisalia dakika kumi tu itimie saa kumi na moja jioni.
Nilitoka chumbani nikaenda ukumbini nikaenda mpaka kaunta nikadai bia nilizoziacha wakanipa bia tatu nikanywa moja zingine nikamwambia mhudumu wa kaunta anywe tu kwani nisingeweza kurudi tena au hata kama ningerudi tena basi ningenunua zingine.
Alishukuru.

Nikaondoka zangu, nikatoka mpaka nje ya bar nikaita bodaboda haraka ikafika moja.
“Nipeleke mjini haraka.”
“Elfu tano!”
“Nini?”
Nilimwangalia kijana yule kwa mshangao!
“Elfu tano tu dada yangu.”
“Sawa.”
Nilijibu hivyo kisha nikaanza kuondoka, niliona kubishana nae isingekuwa busara.
“Mbona unaondoka dada yangu?”
Aliniuliza nami sikumjibu nikazidi kwenda.
Akawasha pikipiki yake akaja na kunipita akasimama kwa mbele.
“Dada kwani we una shilingi ngapi?”
“Sina hela unayotaja tafadhali nipishe!”
“Siyo hivyo dada si tunaongea tu? Au.”
“Elfu mbili unaenda au huendi?”
Nilimuuliza kwa nyodo.
“Naenda.”
“Twende.”
Nikapanda boda ikaondolewa safari ikaanza.
“Unashukia sehemu gani?”
“Nishushe Hope Miyomboni.”
“Maeneo ya sheli?”
“Ndiyo.”
“Poa.”

Baada ya kujua ni wapi nashukia alivuta mafuta kwa wingi sana alivyofika Mlandege round about akaipiga kofi pikipiki ikashuka na mteremko wa mshindo kama upepo vile sekunde chache tukawa tumefika sehemu niliyotaka kushukia.
“Si hapa?”
“Ndiyo.”
Nikashuka mara yule dereva bodaboda akabadili kiswahili.
“Awee dada angu hapa elfu tano haitoshi ongeza buku.”
“Hivi kwani tumekubaliana kiasi gani?”
Nilimuuliza.
“Elfu tano bwana mbona unajisahaulisha?”
“Najisahaulisha siyo? OK.”
Nilimsogelea huku nikitabasamu.
Nilifungua mkoba wangu kisha nikatoa bastola baadala ya pesa kwa usiri mkubwa nikamwonesha.
“Unaiona hii?… Mimi ni mhuni kuliko hata wewe cheza ovyo na mimi utanijua vizuri mimi ni nani nyau wewe!”
Nikarudisha bastola yangu mkobani pasipo mtu mwingine yeyote kuiona licha ya kuwapo watu wengi sana eneo lile.
“Aa…aa, unajua nini dada utanii tu! Hahaha si unajua tena usinichenjie basi hahaha.”
Aliongea kwa kubwabwaja maneno huku akicheka kicheko cha kilio.
Alidata siyo kitoto, aliogopa na kunywea kama puto lililokosa hewa.
Papo hapo nilitoa shilingi elfu kumi na kumpa.
“Haraka nahitaji chenji.”
Nilimfokea.
“Ahaa! OK sasa dada ee shika kwanza hela yako ngoja nichukue chenji kabisa hapo kwa mshikaji nije kuichukua maana hapa chenji ya hiyo ni uchawi.”
Alinirudushia hela yangu akawasha pikipiki akaondoka na asirudi tena.

Nilitabasamu kisha nikaondoka eneo lile moja kwa moja nikaingia NMB Bank sababu haikuwa mbali kutoka niliposhushwa na bodaboda.
Huko niliziingiza zile milioni hamsini kwenye akaunti kisha nilitoka, tayari ilishatimia saa kumi na moja na nusu jioni muda ulikuwa unayoyoma kwelikweli.
Baada ya kutoka benki nilimpigia Sam.
“Hallo.” “Uko wapi Sam?”
“Nipo Mafinga mke wangu vipi?”
“Loh! Umeenda saa ngapi huko tena?”
“Hahaha! Huku tumekuja mida ya saa tisa hivi kuna ajali imetokea maeneo ya lungemba hapa basi limepinduka hivyo tumeombwa kuja kutoa misaada majeruhi wawahishwe hospitali ya rufaa mara moja hapo mjini.”
“Ooh! Vizuri si utarudi lakini?”
“Sasa nilale wapi tena mke wangu jamani?”
“Nikahisi leo utalala kwa malaya wa Mafinga.”
“Hahahaha! Acha zako… Mke baadae basi niko kazini.”
“Sawa baby! Baiii… Ila jitahidi leo tuonane.”
“Usiwaze.”
Nilikata simu, nayo ikawa saa kumi na moja na dakika arobaini.
Nilianza kutembea taratibu sikutaka kuchukua usafiri wowote ingawa nilikuwa na lengo la kupanda moja kwa moja Miami ili niwe wa kwanza kufika kabla ya mhusika.
Nilitembea mpaka Stendi ya zamani huko nikawa natembea taratibu kwa kupoteza muda nikanunua na viulembo vichache kutoka kwa machinga mfano bangili, vipete vidogo viwili pamoja na bangili moja ndogo ya ushanga ambayo kwa kuitizama tu niligundua imetengenezwa na mmasai kwani ilisukwa kwa ustadi mkubwa sana.

Mpaka inatimia saa kumi na mbili na robo jioni bado nilikuwa nazurura tu stendi ya zamani baadae nilipanda bajaji safari ya kwenda Miami bar kupitia barabara ya VETA ikaanza.
Nilianza kupanga mikakati namna nitakavyompoteza kiumbe huyu anaedaiwa kusaliti jumuia ya watu wabaya na wenye pesa na wasiopenda mzaha na siri zao.
Wakati nikiwa kwenye Bajaji nilifungua mkoba nikaifungua pia ile bahasha ndani kwa ndani wakati huo ilibakiwa na picha tu.
Nikaitoa ile picha nikaiweka katikati ya viganja na kuificha ili wa pembeni yangu asiione niliitizama picha ya Abdalah Kizau nikatabasamu na kumpa pole yake maana mauti yalikuwa nyuma yake pasipo yeye kujua.
Nilifika Miami bar ikiwa ni saa kumi na mbili na nusu, nilishuka kwenye bajaji kisha nilimlipa dereva bajaji ujira wake nae akaendelea na safari zake.
Niliingia bar cha kwanza nilienda sehemu ya vyakula uzuri bar hii swala la chakula lilipewa kipaumbele sana.
Huko niliagiza nyama ya kukaangwa nusu pamoja na ugali kidogo maana jioni ile nilijiskia kula ugali, pia niliagiza maziwa.
Baada ya hapo nilimwekeza mpishi sehemu nitakapokuwepo kisha niliondoka zangu.
Nikafika ghorofani nikatafuta sehemu tulivu nikaketi nikatizama kama ukutani mahali nilipoketi kama kuna soketi, yes niliiona basi nilitoa simu na chaja yangu kisha nikaanza kuichaji.
Mhudumu alipofika kunisikiliza niliagiza maji ya Kilimanjaro na Grand Malta moja kubwa, sikutaka kunywa pombe maana nilihisi pombe ingenipotezea mwelekeo wa kazi iliyokuwa mbele yangu.
Baadae nyama na ugali nilioagiza sambamba na maziwa vilifika, bila hiana nilinawishwa na mhudumu taratibu nilianza kula.
Nilikula nikashiba na kubakiza, vyombo nikavisukuma pembeni, punde si punde vikatolewa na meza ikasafishwa.
Nilichomoa simu yangu iliyokuwepo chaji kisha nilimtafuta Sam hewani.

“Ndiyo mke wangu.”
“Bado mpo Mafinga?”
“Hapana… Tupo njia panda ya Tosa tunarudi.”
“Sawa nipo Miami.”
“Nikimaliza shughuli nitakuja, si unalala hapo?”
“Inawezekana lakini sina uhakika.”
“Sawa tuwasiliane hiyo baadae basi.”
“Sawa.”
Nilikata simu na kuirudisha chaji.
Nayo ikawa imetimia saa moja na dakika kumi, mwanga wa mataa ukaanza kuchukua utawala baada ya jua kuzama, hali ilianza kubadilika taratibu mji ulianza kuwa wa baridi baada ya kiza kuanza kuchukua nafasi japo taa ziliendelea kufanya vyema kuhakikisha mji haukumbwi na adha ya giza.
Dakika moja baada ya mimi kukata simu kuna ugeni uliingia.
Alitangulia mwanamke mmoja mzuri hatari, acha tu niseme ukweli mimi ni mwanamke lakini yule mwanamke acheni nimpe sifa zake.
Kwanza alikuwa mzuri wa sura kama Mnyarwanda vile, sasa balaa lipo kwenye shepu…! Mamaaa! Malkia gani huyo mwili uligawanyika vyema kila kiungo kilikaa mahali pake na kwa ukubwa sahihi.
Alikuwa mrefu kwenda hewani kiasi, halafu alikuwa na nywele ndefu mpaka kwenye makalio, tembea yake nayo ilinikosha alitembea mithili ya mrembo fulani aliekuwa anawania taji la mrembo wa dunia katika shindano.
Yaani nilibaki kumtizama tu mwanamke yule.
Mara alipofika usawa fulani ndani ya ukumbi ule uliopo ghorofani alisimama na kuangaza macho pande zote za ukumbi ule wa vinywaji.
Mara alianza kuja meza nilipokuwepo.
Nyuma yake alifatia mwanaume mmoja maji ya kunde mwenye mwili mzuri wa afya alievalia suti nzuri pamoja na kiatu cha hela nyingi.
Begani alivalia begi ndogo nyeusi bila shaka mule ndani kama hakubeba vitabu basi kuna nyaraka alikuwa kazibeba.
Sura ya mwanaume yule ilizirudisha fikra zangu ndani ya mkoba wangu, nikapata kuifananisha sura yake na picha ya Abdalah Kizau, sura iliendana kwa kila kitu kwa mujibu wa kumbukumbu zangu.
Nilishusha pumzi nikatulia.

Wa kwanza kufika mezani ni yule mwanamke, alifika akavuta kiti akaketi, tukasalimiana kwa pamoja kisha waliagiza mvinyo mwekundu walianza na kunywa, walimaliza chupa moja harakaharaka kukata kiu.
Ikaagizwa chupa ya pili.
Dakika kumi mbele wakaanza kulewa, kama ujuavyo baadhi ya mvinyo unavyolewesha haraka.
“Samahani dada naitwa Angel Devil.”
Yule dada alianza kujitambulisha kwangu, kabla ya kumjibu nilimtizama kwanza yule mwanaume… Unajua kwanini nilimtizama?
Ni kwa sababu sauti ya Angel Devil ilisikika masikioni mwangu ndani kabisa karibu na ngoma kana kwamba alininong’onezea masikioni ndani kabisa wakati alikuwa mbali upande wa pili tena kaketi kitini.
Duh!
“Hasikii huyo, mimi ndiye niliejitambulisha kwako!”
Alisema.
“Mimi naitwa Leylah.”
Nilimjibu, wakati ule nilikuwa na wasiwasi sana nilihisi huenda yule mwanaume ataisikia sauti yangu.
Lakini hakuisikia sababu licha ya mimi kuongea hakushtuka wala kugeuka.
“Huyu anaitwa Abdalah Kizau, kazi yako ifanye tukiwa tumetoka hapa sawa?… Nitampeleka bafuni kisha nitamtelekeza huko wewe mfate mmalize sawa?”
Hakika safari hii niliogopa hata kujibu kwa sauti nikaitikia kwa kutikisa kichwa, ingawa sauti yake ilisikika vilevile kama awali ndani kabisa ya masikio yangu kana kwamba maneno hayo yalisikika kwenye spika ndogo za masikio (earphones).
Basi nae yule mwanamke hakuendelea kuniongelesha baadala yake wakawa bize na pombe zao baadae wakalewa vitu vya siri wakaanza kufanya hadharani.

Walianza kufanya mahaba ya ajabuajabu walinyonyana denda baadae Abdalah akitoa ziwa la Angel Devil akaanza kulinyonya.
Mi nikaondoka nikaenda chooni huko nikatoa bastola yangu kuna sehemu nikafungua na kutoa kiwambo nikafunga kisha nilifungua sehemu ya risasi nikaona kuna risasi tano zilizokaa kwenye chemba kwa mipangilio mzuri.
Nikaifunga na kuirudisha kwenye mkoba kisha nilirudi mezani.
Nayo ikawa imetimia saa mbili na dakika arobaini usiku.
Kutokana na ugwadu ambao pangine alikuwa nao Abdalah Kizau juu ya Angel Devil hakutaka kuona muda unaenda zaidi aliondoka muda uleule akaenda kulipia chumba wakati anarudi Angel Devil akaniambia kuwa ni chumba namba 16 Abdalah amechukua.
Nilishangaa Angel hakutoka pale wakati Abdalah anaenda kulipia chumba je, yeye alijuaje kuwa amelipia chumba namba 16?
Mmh!
Nikaacha mambo yaende jinsi yaendavyo.
Abdalah Kizau alivyofika alimchukua Angel wakaondoka, niliwaangalia wanavyoenda huku wakiwa wameshikana viuno mpaka wanapotelea huku nyuma nilimwonea huruma mwanaume yule kwani hakujua kuwa nyuma yake kifo kilikuwa kinamfata.
Nilitulia ndani ya dakika kumi nikasoma mazingira nikaona wahudumu wamezubaa hata wa vyumba hakuwepo sijui alikuwa ameenda showtime, mimi sijui.
Pale pale nilitoka ghafla kama mwizi anaelekea kufanya ukwapuzi, nikafika chumba namba 16 kilikuwa hakijafungwa mlango ulikuwa umerudishiwa tu.
Nikausukuma huku nikitoa bastola na kuikamata vyema mkononi, nilivyoingia ndani nikakuta kitanda kitupu ila nguo na kibegu cha Abdalah kizau kilikuwepo.
Nikasimama kwanza mara nikamsikia anamwita Angel akiwa bafuni kama unavyojua vyumba vya VIP huwa vina vyoo na bafu ndani kwa ndani, na nilivyotizama upande wa kulia mwa kitanda niliuona mlango wa kuelekea ilipo bafu na choo nao ulikuwa haujafungwa zaidi ya kurudishiwa tu.
Bila kufanya ajizi nilienda pale na kuufungua mlango kwa nguvu vuup! Bastola ikiwa imetangulia…
Hamadi huyu hapa Abdalah kizau akiwa kajipaka povu la sabuni mwili mzima huku akimwita Angel Devil ambae bila shaka alikuwa chooni.
Macho yalimtoka pima shuzi kubwa likamtoka kwa sauti baada ya kuona kibomba cha bastola kikiwa kimeelekea kwenye paji lake la uso.

Sehemu 20 Sehemu 22
0
0