Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Dunia Ya Pili - 06

Nilijiuliza.
“Hizi ni pombe au?”
Bado sikupata jibu.
Wakati nikiwa nimeduwaa na butwaa lile, Sam yeye alimimina pombe kwenye glasi hadi ikajaa kisha akaipeleka mdomoni akapiga funda tatu kisha akaitua mezani.
“Vipi mrembo mbona umeduwaa? Ee? Au uzuri wa bar umekuchanganya?”
Aliuliza Sam huku sauti yake ilionesha wazi ameshaanza kulewa wine.
“Sam huoni wale watu wanaojamiiana hadharani?”
Nilimuuliza huku nilitegemea nae atashituka kama nilivyoshituka mimi.
“Hahahahahahaha…”
Sam alicheka sana.
“Usiogope Leylah! Katika ulimwengu wetu hakuna siri vitu vyote hufanyika hadharani.”
Alisema.
Nikazidi kushangaa.
“Kwanini?”
Nilihoji.
“Kwanini iwe siri?”
Sam nae akanihoji.
Saa hiyo akichukua glasi ya wine na kuipeleka mdomoni, wine iliyokuwa imebakia kwenye glasi akaimiminia yote kisha akatua glasi tupu mezani.
“Hakuna siri hata huko kwenye dunia yenu bali kinachoendelea kwenye dunia yenu ni uongo uliokubuhu kuhusu dhana ya siri hizo, jiulize kujamiiana ingekuwa jambo baya watu wangekuwa wanaoana na kuzaliana? Na kama ni siri kwanini wanyama hujamiiana hadharani? Kwamba wao hawana siri? Aaah!”
Sam alirusha mkono hewani kwa dharau kisha akachukua chupa ya wine akaimiminia pombe kwenye glasi mpaka ikajaa tena akatua chupa, akaokota glasi akaiweka mdomoni akaishusha glasi ile mpaka nusu akaishusha kisha alianza kucheza mziki akiwa kaketi pale pale kitini.
Nikabaki namtizma tu.
“Kunywa Leylah nataka kuagiza vinywaji vingine mrembo vipiiii? Au unataka misosi? Sema!”
Aliongea Sam huku akiokota glasi akanipatia, nikaipokea.
“Halafu we Sam uliniwekea pombe kwenye kinywaji changu wakati nilipokuwa bize na simu wewe!”
Niliongea wakati huo nikipeleka kinywaji mdomoni.
“Awee! Sijafanya hivyo mimi.”
“Tabia mbaya!”
“Wala.”

Mara simu yangu ikaita!
Kwanza nilishituka nikajiuliza ni nani mwenye namba yangu wakati simu nimenunua leo tu na hakuna mtu niliebadilishana nae namba?
“Mhh!”
Niliiokota kisha nikatizama kwenye kioo kujua ni nani mpigaji.
“Sh. Jemima…”
Namba kutoka mtandao wa Vodacom ilikuja ikiwa imeseviwa kabisa jina la shangazi yangu Jemima.
Nilishtuka siyo kidogo, hasa nilivyokumbuka kuwa kuna wakati niliangalia status yake WhatsApp.
Nilimtizama Sam nikaona yupo bize kabisa hata hakutilia maanani simu yangu ilivyokuwa inaita.
Maamuzi ya kupokea yakanijia!
Nikaweka kidole na kutelezeshea kwenye kitufe cha kijani, simu ikapokelewa.
“Hallo!”
“Habari yako.”
Alisikika shangazi akinisalimia, tumbo likakata waah… Hadi nikashituka.
“Safi.”
Nilijibu kifupi huku nisijue mbeleni nitajibu nini.
“Uko wapi?”
Aliuliza.
Hilo swali nililitegemea.
Sikuwa na jibu la kumpa hivyo nilikaa kimya, ghafla Sam alinipora simu yangu kisha aliiweka sikioni kwake.
“Habari… Naitwa inspekta Sam, Leylah yupo kituo kikuu cha polisi Iringa mjini, ameshikiriwa kwa uchunguzi na mahojiano maalum hivyo ataachiliwa baada ya upelelezi kukamilika.”
Aliongea Sam kisha bila hata kusikiliza upande wa pili alikata simu huku akibetua midomo yake kwa dharau akanirushia simu yangu…
Niliidaka kwa heshima kama yai.
“Kula vitu Leylah, wewe ni bilionea mtarajiwa hivyo kuwa huru usikubali mtu akusumbue tambua upo chini ya ulimwengu wenye nguvu kubwa sana hahahahaha…!”
Alicheka Sam mwenyewe kwa maneno yake kisha aliokota glasi ya pombe akaendelea kumwagilia moyo.
Nami niliokota yangu nikaiweka mdomoni nikapiga funda tatu za maana, safari hii nilihisi radha ya tofauti mdomoni nilikutana na radha ya pombe kabisa.
“Sam…!”
Niliita kwa hasira huku nikiweka glasi mezani kwa nguvu.
“Vipi?”
Aliuliza.
“Sinywi mimi tena vinywaji vyako kunywa mwenyewe!”
Nilizila nikachukua simu yangu nikaendelea kuperuzi mtandaoni, nilifungua account ya Facebook, huko nikajiunga na makundi kadhaa ya udaku, vichekesho, na kadhalika…
Papo hapo nilijipiga picha kali kadhaa nikiwa bar nikachagua moja nzuri nikaiweka kwenye wasifu, kisha nyingine niliipost kawaida.
Nikatoka facebook nikaingia WhatsApp nako nikaiweka picha moja kwenye wasifu na nyingine nikaweka status, nikisahau kuwa muda mfupi nimeongea na shangazi na akapewa taarifa ya uongo kuwa nipo kituo cha polisi sasa hii ya kujipost niko bar?
Muda huo huo ujumbe ukaingia WhatsApp.
“Ahaaa! Hapo ndiyo kituo cha polisi siyo ee?”
Nilishituka sana baada ya kusoma ujumbe ule kutoka kwa shangazi, niliishiwa pozi si kawaida nikahisi kichwa kinaanza kuuma, hamu ya kuperuzi iliisha nikahisi kuumwa.

Ni kama kuna kumbukumbu ya kushitua ilinijia kichwani ndiyo maana nilijikuta na hali hiyo.
Nikaweka simu mezani huku nikishusha pumzi nyepesi ya mashaka.
“Vipi?”
Aliniuliza Sam.
“Walaa.”
Nilimkana.
“Leylah ujue unaniangusha sana unaposhindwa kujiamini… Kwanini unakuwa hivyo?”
Aliongea Sam maneno ambayo yaliniacha njia panda.
Nikamuuliza.
“Kwanini?”
“Sikia, Unajua wazi una kesi ya mauaji siyo?… Sisi ndiyo tulikutoa eneo la tukio ili wananchi wenye hasira kali wasikudhuru au kukuua kabisa, kupotea kwako katika mazingira yale kulimstaajabisha kila mmoja hata wale wanga wakubwa katika eneo lile waliogopa sana kwa kile kilichotokea, sasa nakushangaa unaposhindwa kujiamini kwaninii?”
Aliongea Sam kwa sauti ya msisitizo.
Maneno yake yakafanya kumbukumbu nyingi zirudi kwa kasi, nilikumbuka mlolongo mzima wa tukio lile hadi kukimbia kwangu, na mwisho sikujua kilichotokea baada ya kuzingirwa na kundi kubwa la mbwa na watu.
Baadae nikajikuta mazingira mengine nikiwa na kiumbe Soul ambae alijitambulisha kwangu kwa jina la Sauli.

Nilimwangalia Sam usoni, nilitamani kumuambia kitu lakini cha kumuambia nilikosa, kila nilichofikiria kuongea kilisahaulika muda huo huo.
Kichwa changu kikageuka memory yenye virus yaani kila nilichowaza nilisahau papo hapo nikawaza kingine.
Baadae niliokota simu yangu, kuwasha kioo nilikutana na ujumbe ambao uliingia kwa njia ya kawaida, nilitoa lock ya simu kisha niliufungua.
Sawa nawe potea kabisa tusije kukuona utakiona cha moto, pia tutaomba mabaya kwajili yako, nawe lolote baya lazima likukute wifi.
Ujumbe huu ulitumwa kutoka kwa wifi yangu Stella, Stella nilikuwa sipatani nae hivyo ujumbe wake ulinipa kisirani nikajikuta naokota glasi niliyokuwa nimeisusa nikamimina kinywaji chote nikaishusha ikiwa tupu.
Papo hapo tumbo lilipokelea…
Huwezi amini kumbe niliokota pombe tupu nikainywa afadhali hata za mwanzo Sam alikuwa ananichanganyia kwenye Malta.
“Haa! We Leylah unakunywaje hivyo pombe au umelewa?”
Sam aliniuliza huku akitizama kwa tahamaki.
Hata sikuelewa anaongea nini, ile pombe ilinipanda ndani ya muda mfupi, nikajikuta nanyanyuka na kuanza kucheza mziki huku nikijirekodi video na picha juu sikutaka tena maelezo na mtu!.
Ama kweli pombe siyo chai.
Kutokana na muziki mnene uliokuwa ukidunda mle ndani ya ukumbi wa ile bar jumlisha na pombe niliyokunywa kwa fujo nikajikuta nazidiwa haraka sana na pombe nikaanza kuhisi kizunguzungu.
Fahamu zikaanza kupotea baadae nilipoteza kabisa kumbukumbu sikujua kilichoendelea.

Nilifumbua macho nikajikuta kitandani…
Nilishangaa, kuangalia pembeni nikimwona Sam akiwa kalala fofofo!
Kuangaza macho huku na kule niliona meza pembeni yetu, juu yake zikiwa zimewekwa chupa tano za wine, tatu za Malta na hotpot moja kubwa!
Nikameza mate kuona hotpot lile.
Pembeni ya hotpot ile lilikuwepo burungutu kubwa sana la hela! Nilijikuta nakenua meno kuliona burungutu hilo.
Nikaendelea kukisabahi chumba kile kila kona mara naona saa kubwa ya mshale ukutani ikiendelea kuzunguka taratibu huku ikisona saa moja na dakika kumi na tano asubuhi.
“Kumbe kumekucha?”
Nilijiuliza hivyo saa hiyo nikishuka kitanda nikiwa na night dress, nikatembea mpaka dirisha nikafunua pazia na kuangalia nje.
Kweli kulikuwa kumekucha na harakati za mjini zilikuwa zinaendelea kama kawaida, ila sasa cha kushangaza jua nilikuwa silioni zaidi ya mwanga tu.
“Mh!”
Niliguna kimoyo moyo kisha nikageuka, Sam ndiyo alikuwa akijinyoosha kitandani.
“Mambo Sam umeamkaje?”
“Safi Leylah nimeamka salama kabisa hofu kwako.”
“Nami pia nimeamka salama!”
“Basi vizuri.”
Wote tukawa tumeamka, Sam alinionesha bafu, nikaingia huko nikaoga safi nikatoka, Sam nae aliingia akaoga akatoka alinikuta nimeshavaa viwalo vyangu wakati huo nipo najipulizia unyunyu.
Nae vile vile alifika akabadilika.
“Fungua hilo hotpot Leylah.”
Alisema Sam, nami ndicho nilichokuwa nakisubili tu.
Nilifungua kwa papara, nikajikuta natabasamu mwenyewe.
Humo ndani ilikuwepo supu ya kutakata!
Ikiwa kwenye vihotpot vidogo viwili vilivyopangwa ndani sambamba na chapati sita zilizofunikwa vyema na gazeti, yaani tatu kwa kila mtu.
Nilifurahi mno! Basi kwa pamoja tulipata supu ile.
Baada ya hapo Sam aliniuliza kama nahitaji kupata kinywaji.
Nilimjibu kuwa sikuwa najisikia kunywa kinywaji chochote wakati ule.
Basi Sam akanipa maelekezo machache pale, kisha alichukua lile burungutu la pesa lililokuwa pale mezani akanifungia kwenye gazeti lililokuwa limetumika kufungia chapati, halafu akanikabidhi.
“Chukua hii, mambo mengine utakutana nayo mbele ya safari sawa ee…”
“Sawa.”
Nilimjibu.
“Tutakutana huko!”
“Ok.”

Nilinyanyuka…
Kitendo cha kusimama tu nikajikuta nipo maeneo ya TANESCO Iringa mjini nikiwa natembea kuelekea kusini mwa mji nikifata barabara kuu ya mji, mkono wa kushoto nikiwa nimeshika gazeti lililoviringishwa pesa, huku mkono wa kulia nikiwa nimeshika simu yangu.
Nilitembea nilivyofika mbele kidogo baada ya kupita ofisi ya TANESCO nilikutana na barabara iliyokuwa ikitokea magharibi ikielekea mashabiki, nikaunga nayo hiyo ambayo ilinipeleka moja kwa moja mpaka maduka ya Miyomboni.
Huko nilichagua duka moja la mabegi na mikoba, nikaingia humo nikanunua mkoba mmoja mdogo nikalifungua gezeti langu mbele ya muuza mabegi nikachukua lile burungutu la pesa na kuliweka ndani ya mkoba kisha niliaga nikageuka na kuanza kutembea kuelekea nje.
Nilipiga hatua tatu kisha niligeuka nyuma nikaona yule alieniuzia mkoba akiongea na simu.

Sehemu 5 Sehemu 7
0
0