Dunia Ya Pili - 20
Isingelikuwa eneo la halaiki kitambo sana ningeshamuingiza shaba mwilini mwake bahati kwake mazingira yakawa hatarishi,nilimchukia sana
Skobe nilimchukia vibaya mno! Nilimfananisha na kiumbe fulani wa kutisha!
Nilishusha pumzi kisha nikaokota chupa ya bia nikanywa na kutua mezani.
“Ujue nini Leylah… Najua unanichukia sana kuna siku isiyo na jina utakuja kunishukuru.”
Aliongea Skobe huku nikiona mkono wake wa kushoto unanyanyuka! Nikawa makini zaidi kumkazia macho.
Akaitizama saa yake ya mkononi, kisha alitizama nje kupitia dirisha nililokunjwa pazia.
“Halafu kingine naomba namba yako Leylah.”
Nilimkata jicho kali ingawa hakushtuka.
Mara simu yake ikaita mfukoni, Skobe akatikisa rasta zake kidogo kisha aliingiza mkono mfukoni akatoa simu yake.
Alivyoitizama kwenye kioo,nilishangaa baadala ya kupokea aliangalia tena saa yake kwa mara ya pili kisha macho yake akayelekeza nje kupitia
dirisha lililokunjwa pazia, huko akayatuliza macho yake ndani ya sekunde kadhaa wakati huo simu yake ikiendelea kuita pasipo kupokelewa.
Ghafla alitoa bastola!
Nikashituka nami nikavuta ya kwangu lakini yangu niliificha kwenye mapaja!
Sikuitoa hadharani.
Yaani kitendo cha kufumba na kufumbua Skobe alihama eneo lile kwa namna ya kutisha!
Niseme tu ukweli namna Skobe alivyoondoka pale ilitisha!
Aliruka akapita juu ya meza ile anatua upande mwingine nikashituka kuona kamba ya chaja ikitua mezani peke yake ikitokea kwa juu!
Wakati huo yeye alipotelea upande wa majikoni.
Kushtuka simu hamna! Nikapigwa bumbuwazi!
Nilishindwa hata kupiga mayowe nikabaki nimeganda kama sanamu.
Muda huohuo polisi waliingia mule ndani, wakapitiliza mpaka eneo la majikoni wanakopikia wahudumu wa bar hiyo ila cha
ajabu walirudi wao kama wao! Skobe hakuwepo tena.
“Aisee wakati nafika kule majikoni nilimuona yupo juu ya paa la jiko hilo cha ajabu nilipoongea na Sam kupitia simu ya upepo
aliniambia muda huo wanaongea jamaa keshatua nje kitambo na kaingia vichochoroni hivyo imekuwa ngumu kumfukuzia.”
Walisikika wale polisi wakiongea baada ya kumkosa Skobe!
Niliwaza unajua?
Niliwaza sana huyu ni mtu wa aina gani? Ni mazoezi gani aliyonayo hata kufanya vitu vya kuogopeka namna hii?
Walai nilijiuliza lakini jawabu sikulipata.
Simu yangu iliondoka ikabidi tu nianze kupanga ratiba za kununua nyingine kwani jinsi simu hiyo ilivyochukuliwa hata msaada nilishindwa kuomba!
Baadae kama dakika kumi hivi baada ya polisi kuondoka Skobe alirudi tena alitokea upande uleule wa majikoni alikotokomea awali.
Kikukweli mshangao niliobaki nao moyoni hauwezi hata kuelezeka.
“Skobe!”
Nilimwita pindi amefika mahali nilipokuwepo.
“Niambie Leylah… simu yako hii hapa samahani kwa kuondoka nayo bila ridhaa yako lakini nilikuwa napiga nilikuwa na shida muhimu halafu
sikuwa na salio hasa baada ya polisi kufika eneo hili.”
Yaani nilimwangalia mwanaume yule nilishindwa kummaliza.
“Wewe si ulikuwa unaongea na simu hapa au?”
Niliuliza kwa sauti ya mlipuko! Kihoro cha hasira kilishanikaa kifuani.
“Nilipigiwa.”
Alijibu kwa sauti ya taratibu kabisa.
“Mchoro wa kufuli umetoaje kwenye simu yangu?”
“Mmh! Sasa nawe hilo ni swali la kuniuliza Leylah… Wewe mimi IT ipo kichwani.”
Nilimwangalia Skobe kiufupi kila alichonijibu kiliniongezea hasira tu mwisho niliamua kumuacha nikachukua simu yangu mkononi mwake na
kuiweka moja kwa moja kwenye mkoba, sikutaka tena hata kuendelea kuiachaji.
Skobe aliaga akaanza kuondoka…
“Skobe!”
Nilimwita nae akageuga na kurudi.
“Nambie.”
“Kwanini polisi wanakutafuta sana?… Una kosa gani haswa?”
Nilimuuliza.
“Hayo siyo ya kuyazungumzia sehemu kama hii… Halafu OK nimekumbuka kitu Leylah.”
Aliongea hivyo huku akirudi kitini.
Akaketi kitini, macho yake kwa mara nyingine tena aliyaelekeza dirisha alilokuwa akilitizama mwanzo kabla hajakimbizwa na askari polisi.
Baadae alirudisha uso wake akanitizama usoni.
“Najua kesho una safari ya kwenda Dar es salaam, unakwenda kuwa staa mkubwa sana hapa nchini na hata nje ya nchi,
kiufupi unakwenda kuwa staa mkubwa duniani…
Unajua nini? Ukiona dunia imekutizama hata mara moja tu kupitia runinga ujue wewe tayari ni mtu maarufu…
Sasa nina ushauri mmoja kwako Leylah… Wewe unakwenda kuwa mtu maarufu hapa nchini sawa? Sasa tumia fursa hiyo kutafuta sana pesa… Ujue nini?”
Aliweka kituo kwanza, akatizama pande zote kuona kama kuna ambae anaweza kuwa anatusikia, akaona kupo shwari kila mmoja anashughulika na unywaji tu.
Akaendelea.
“Sikia… pindi utakapokuwa Dar es salaam baada filamu yenu moja kutoka na kusambaa mitandaoni baadae utakutana na tajiri mmoja mkubwa sana…
Katika kukutana kwenu kutatokea mambo makubwa sana na kama utaitumia vizuri fursa hiyo basi utatengeneza mabilioni ya pesa hata utaamua
kuachana na uigizaji… Ni hayo tu!”
Kisha Skobe aliondoka zake akaniacha ndani ya tafakari kuu.
Nilimtizama Skobe mpaka anapotelea mlangoni akatokomea nje, yaani nilishindwa kuelewa kilichokuwa kinaendelea, mtu ambaye alikuwa anajiamini kwa
kiasi ambacho siyo cha kawaida halafu mbaya zaidi akawa na uwezo usio wa kawaida kabisa kuanzia kutafakari hata utendaji pia.
“Mmh! Ukute Skobe nae ndiyo walewale kina Samweli.”
Nilijiongelea moyoni kisha nilichukua chupa ya bia nikanywa na kutua mezani.
Hatimae ikatimia saa sita na nusu mchana, nilihisi njaa hivyo ilinibidi nikabidhi bia zilizobaki kwa mhudumu mmoja hapo bar
ili nitoke nitafute chakula kwanza.
Nilitoka mpaka nje, sikuwa napendele kula mahotelini japo uwezo huo nilikuwa nao, hivyo mitaa ileile nilitafuta mgahawa uliokuwa karibu
nikaingia hapo, nilikutana na mhudumu mama wa makamo kiasi.
“Karibu.”
“Asante mama shikamoo!”
Nilimpa heshima yake.
“Marhaba karibu.”
Niliketi kitini, punde si punde alikuja kunisikiliza lakini kitendo cha kunisogelea tu!
Aligandisha macho yake usoni kwangu hata nywele zangu zikasisimka.
“Huyu mama mbona ananitizama hivi?”
Nilijiuliza.
“Karibu nakusikiliza.”
Aliongea pindi nimemaliza kujiuliza moyoni.
“Nasubili kupata orodha ya vyakula ilivyotupikia leo nipate kuchagua.”
Nilimjibu.
“Sawa, hapa kuna wali nyama, wali samaki, maharage kwa mboga za majani, pia kuna ugali na mboga nilizokutajia,
kuna pilau, ugali wa mhogo, ugali wa viazi, maziwa, chai, na vitafunwa vyote muhimu… Bei ya vyakula ni kuanzia elfu moja mia tano,
na chai kwa vitafunwa ni kuanzia elfu moja.”
“Ooh! Sawa asante naomba wali samaki wa shilingi elfu mbili.”
“Sawa.”
Yule mama akaenda kwenye masufuria ya vyakula.
Mama wee!
Alivyofunya sufuria la wali nilishituka kuona siyo wali bali ni unga wa mbo uliochanganywa na vitu vigeni kabisa machoni pangu!
Mmh! Nikajikausha kwanza, akapakua hicho chakula katika sahani kisha akafunika na kufunua sufuria lenye mchuzi na samaki.
Toba! Nilishangaa kuona ni damu mbichi na vipande vya nyoka vilivyokatwa katwa.
“Samahani mama hebu funua kwanza sufuria la ugali huenda nikapenda pia ugali.”
Niliongea huku nikinyanyuka na kuisogelea meza ile kubwa iliyotengwa masufuria ya vyakula.
Akafunua sufuria ya ugali.
Duuh! Nilitamani kutapika baada ya kuona kinyesi kikubwa cha binadamu ndani ya sufuria na si ugali.
Nilighairi ghafla.
“Mama asante nimeghairi kula, kuna ujumbe wa dharura hapa nimepata samahani sana kwa usumbufu.”
Niliongea huku nikionekana kuwa na haraka kweli na simu ikiwa mkononi.
Yule mama pasipo kunijibu alifunika chakula haraka kisha akanisogelea na kunitizama kwa ukaribu zaidi.
“Najua kilichokughairisha sasa iwe siri yako sawa?”
“Amna mama…”
Nilijitetea.
“Weweee huwezi kunidanganya kwa chochote macho yako yanaonesha wazi wewe ni mtukutu ndiyo maana nikakuambua koma na iwe siri yako sawa?”
Aliongea huku akinikazia macho yake makali, siyo siri mama yule alibadilika sana.
“Sawa…Sawa mama nimekuelewa ondoa shaka kuhusu mimi.”
Nilizidi kujitetea.
“Nenda.”
Aliniruhusu.
Nikatoka nje ya mgahawa wake, siyo siri nilichokiona mgahawani pa mama yule kiliniharibu mtima wangu moja kwa moja hata hamu ya kula ikanitoka.
“Kumbe kuna watu wachawi jamani loh!”
Nilitoka hapo nikatembea na uchochoro fulani hivi hatimae nikaja kutokea mwisho wa lami hapo nilijitosa barabarani nikachukua bodaboda moja
iliyonikimbiza mpaka Iringa mjini ndani huko nilitafuta mgahawa mmoja mzuri msafi na wenye hadhi nikaingia huko.
Nikala kisha nilitoka na kuchukua bodaboda iliyonirudisha moja kwa moja Serengeti bar.
Nayo ikawa imetimia saa nane kasoro dakika kumi mchana.
Nilihisi uchovu mchana ule baada ya chakula hivyo ilinibidi nichukue chumba kwanza ili nipumzike hapohapo bar.
Baada ya kuchukua chumba niliingia huko nikahifadhi mkoba wangu kisha nilipunguza nguo nikajifunga taulo nikaingia bafuni huko nikaoga
vyema kuondoa jasho sehemu zote za mwili kisha nilirudi chumbani.
Huko nikajipaka mafuta nikajipulizia unyunyu kidogo, nikapulizia na godoro pamoja na shuka kisha nikalala nikajifunika na shuka..\n
Nikiwa kitandani nilianza kuyatafakari maneno ya Skobe.
“Najua kesho una safari ya kwenda Dar es salaam, unakwenda kuwa staa mkubwa sana hapa nchini na hata nje ya nchi, kiufupi unakwenda kuwa staa mkubwa duniani… Unajua nini? Ukiona dunia imekutizama hata mara moja tu kupitia runinga ujue wewe tayari ni mtu maarufu… Sasa nina ushauri mmoja kwako Leylah… Wewe unakwenda kuwa mtu maarufu hapa nchini sawa? Sasa tumia fursa hiyo kutafuta sana pesa… Ujue nini?”
“Sikia… pindi utakapokuwa Dar es salaam baada filamu yenu moja kutoka na kusambaa mitandaoni baadae utakutana na tajiri mmoja mkubwa sana… Katika kukutana kwenu kutatokea mambo makubwa sana na kama utaitumia vizuri fursa hiyo basi utatengeneza mabilioni ya pesa hata utaamua kuachana na uigizaji… Ni hayo tu!”
Niliyafikiria mara mbilimbili maneno ya Skobe halafu ni kama sikuyaelewa vile.
Nilijiuliza sana huyu tajiri atakuwa ni nani?
Ni mambo yapi yatapata kutokea? Na yeye ameyajuaje haya?
Nilijiuliza pasipo kupata majibu hata baadae usingizi ukanijia nikalala.
Mara ilinijia ndoto wakati niko usingizini,niliota nikiwa na Sam pamoja na Skobe tukiwa katika misitu huko Beralus karibu na mipaka ya
Beralus na Urusi hii ni baada ya kufanya biashara haramu ya madini, viungo vya watu na pembe za baadhi wanyama pamoja na kwato zao.
Sasa tulikuwa katika harakati za kurejea Tanzania sasa kwa bahati mbaya kukatokea hitilafu fulani usafiri ukakwama tukafumaniwa na wanamgambo
wa kundi la ‘Islamic State’ wakiwa na taarifa kamili kuhusu sisi wakatuvamia kutaka kupora pesa nyingi tulizonazo.
Kukazuka mapigano makali mapigano yaliyodumu kwa zaidi ya lisaa lizima huku Skobe akionekana kuwathibiti kwa kiasi kikubwa kwa kutumia bunduki
kubwa na ya kisasa aina ya ‘Machine gun M60’.
Mara katika harakati zile Sam anakutana na mauti ya ghafla baada ya kundunguliwa na mlengaji wa masafa marefu kwa risasi ya kichwa!
Nilipiga yowe kali la maumivu mara usingizi ukakata ghafla, nilikurupuka kitandani huku moyo ukidunda kwa nguvu jasho nalo likiwa
limeweka vitone baadhi ya sehemu za mwili.
“Mmh! Ndoto gani tena hizi?”
Nilijuliza nikafyonza kisha nilijifunika shuka nikaendelea kuutafuta usingizi.
Moyo ukiendelea kupwita kwa kasi baadae ukaanza kupunguza kasi, ndipo nikaanza kuona macho nayo yanaanza kuwa mazito zilikuwa ni dalili za
usingizi, hata nilivyojaribu kuyafumbua nikajikuta nipo mji mwingine tena nipo natembea nisijue hata naelekea wapi?
Ulikuwa ni mji mzuri kama Mumbai, majengo marefu, barabara nzuri, hata mpangilio wa ujenzi pia ulikuwa mzuri kiufupi mji ulikuwa unapendeza.
Nikiwa natembea huku nashangaa mara nilisikia simu yangu inaita.
Nikaitoa na kuangalia mpigaji ni nani?
Sam.
Nikapokea.
“Hallo.”
“Upo wapi Leylah?”
“Hapaaa… Mmmh nahisi ni blood tower hili eneo.”
“Sawa nakuja kukuchukua.”
Yaani ile kukata simu tu nashangaa Land lover inapita karibu yangu kisha ikapaki mbele kidogo, niliijua kuwa ile ni gari ya Sam.
Baada ya kupakia alishuka akaja kunilaki.
“Mambo.”
“Safi mzima?”
“Mi' mzima hofu kwako.”
“Mimi pia niko ivoivo.”
Tuliingia garini kisha akaanza kiliendesha taratibu huku tukipiga stori.
“Leo usiku kwa saa za duniani kiongozi anataka kukupa kazi moja kubwa sana…
Hiyo kazi ukiifanikisha hakika utajipatia mamilioni mengine mengi tu, halafu kingine Filamu utakayokwenda kushiriki kuitoa itasambaa
kwa kasi kubwa sana duniani, pia itakufanya uwe maarufu zaidi na bilionea mwenye pesa nyingi sana.”
“Kazi! Kazi ipi hiyo?”
“Twende uonane na kiongozi wetu ujue ni jukumu gani atakupatia leo ila kwa taarifa nilizonazo siyo chini ya milioni mia
utalamba baada ya kazi hiyo pia nyota yako itaongezeka hadhi mara dufu.”
Alipokwisha kuongea hivyo Sam alibadili gia gari ikaanza kwenda kwa kasi kidogo, mara ile kufumbua na kufumbua nikashituka
Sam keshapaki gari kwenye maegesho ndani ya ngome kuu ya Lucifer huko kuzimu na sasa ilikuwa inatakiwa tushuke ili tukaonane na
Lucifer nikapate maagizo juu ya kazi yangu niliyotakiwa kwenda kuifanya usiku wa siku hiyo.
Unaweza pia kusoma: