Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Dunia Ya Pili - 23

Lilikuwa jicho la ulevi na si jicho la taharuki.
“Damson Mbalangu yule tajiri mwenye kanisa pale Manzese?”
Hapo nilikosa chaguo ilibidi tu nijibu...
“Ndiyo.”
Japo sikuwa na uhakika kama anaweza kuwa mwenyewe.
“Ndiyo nampata.”
Nilishusha pumzi,sasa nilianza kuuona mwanga wa kuifanikisha kazi yangu,hapo nikafikiri nianze kuwaza ni kwa jinsi gani ningeweza kujua mienendo yake huyo mwanaume ili iwe rahisi zaidi kumwangamiza.
“Kanisa lake lipo Manzese sehemu gani? Kwa sababu yeye ninamfahamu tu kupitia sifa zake za uinjilishaji lakini simfahamu kiundani zaidi.”
Nilitolea maelezo kidogo katika swali langu.
“Ahaa! Kanisa lake lipo pale Manzese karibu na darajani.”
Alijibu, nikashusha pumzi ya chini chini,nilishaanza kupata mwelekeo mzuri kabisa wa kazi yangu.
Nilifurahi moyoni.
“Damson Mbalangu! Pole kwa lijalo juu yako.”
Nilijisemea moyoni saa hiyo nikichezesha vidole vyangu vya mkono wa kushoto.
“Sawa nashukuru kwa ushirikiano wako Jr.”
“Tuko pamoja dada angu hata sikunyingine ukihitaji pia ushirikiano wangu utapata bila shida kabisa.”
Kitu kingine nilichokigundua kwa Jr licha ya kuonekana amelewa lakini hakuweza kuchanganya herufi katika matamshi yake hii ilinistaajabisha sana.
Unajua ni asilimia kubwa ya watumiaji wa pombe wana kawaida ya kubwabwaja maneno wakilewa lakini hili kwa Jr halikwepo halafu pombe alikuwa akizitupia kama kawaida, mezani mpaka wakati huo ilikuwa imesalia chupa moja kwa upande wake.

Tuliendelea kunywa huku tukipiga soga hatimae usiku ukawa mwingi pombe nazo tukawa tumetosheka nazo kilichofuata ilikuwa ni kulala.
“Jr unalala humu humu au?”
Nilimuuliza nikiwa na kusudi langu.
“Ah! Ujue nini dada, nimekupenda sana, najua wewe siyo malaya na una ndoa yako lakini Dah! Niwe tu muwazi kwako nimekutamani sana tena sana!”
Jr aliropoka ujinga ule pasi na kupepesa wala kujikanyaga!
Halafu aliongea kwa utulivu mkubwa sana huku akichezesha kizibo cha chupa mkononi mwake.
“Ndicho kilichofanya unilipie bia siyo?”
Nilimuuliza kwa sauti ngumu kidogo huku nikiwa nimemkazia jicho!
Akaduwaa!
Nilichokifanya ni kutoa shilingi elfu hamsini kisha nikamrushia kwa dharau kisha niliondoka nikaenda zangu chumbani kwangu nikajifungia na kulala.
Nikiwa usingizini nilijiwa na ndoto moja ya kutisha mno!
Naweza kusema ilikuwa ni ndoto nyingine tena iliyokwenda kufungua ukurasa mpya wa maisha yangu ukiachilia ndoto inayofanana na hiyo niliyowahi kuiota mwanzo.
Unajua ilikuwa ndoto gani hiyo?
Hii apa.

Nikiwa katikati ya msitu mmoja mkubwa ndani ya mkoa wa Iringa ni msitu ambao naufahamu vizuri sana kwani hauko mbali na mji, nilikutana na bibi yangu ambae alifariki zamani sana ni bibi yangu mzaa mama.
Nilikutana nae chini ya mti mkubwa sana wa mkuyu akiwa kajitwisha chungu cheusi tiii kichwani.
Bila hata kusalimiana bibi alianza kuongea.
“Mjukuu wangu Leylah… Umeingia katika agano gumu mno! Upande wa ukoo wako! Lakini pia kuna agano linakusubili upande wa mama yako!
Mama yako aliniambia wewe ndiye mwanae mpendwa utakaemiliki mikoba yake, lakini kwa bahati mbaya alifariki pasipo kukumilikisha mikoba hiyo sababu ulikuwa bado mdogo.”

Aliongea akaweka kituo.
Nikaendelea kumsikiliza.
“Na sasa wakati ni huu! Mizimu inahitaji umiliki wako kwao nami nakufanyia tambiko hapa chini ya mkuyu ukawe mtu mwenye nguvu, tajiri pia mwenye nguvu kimamlaka kwa watu wote waliochini yako! Nitakupatia hilizi, ni hilizi ambayo itakuwezesha kuwasiliana nasi muda wowote utakao, utaomba chochote utapewa lakini kwa sharti moja tu! Kila ifikapo tarehe saba mwezi wa saba itakubidi usafiri mpaka Lupembe kunako mkoa wao Njombe, kuna mkubwa wetu huko atakufanyia miungu midogo midogo na utazidi kuimarika kiuchumi hata kinguvu pia!”
Bibi alipokwisha kuongea hayo alinisogelea akanishikisha hilizi kinguvu mkononi kisha muda huohuo ilipiga radi kubwa bibi akapotea nami nikazinduka usingizini.

Niliinuka kwa kasi kitandani huku moyo ukidunda mfululizo, sambamba na jasho baadhi ya sehemu za mwili.
Nilishusha pumzi nzito mara nikahisi kama nimeshika kitu mkononi mwangu!
Ee! Kuangalia duu! Niliogopa nikatupa pembeni, lilikuwa ni dubwana fulani kuubwa lenye mwonekano wa kutisha! Halafu linahema taratibu!
Haa! Kumbe ni hirizi, nilishtuka nilipoyakumbuka maneno ya bibi ndotoni ilibidi niokote haraka maana nisije nikaadhibiwa na mizimu kwa kuitupa hirizi chini.
Niliiangalia Hirizi ile nikajikuta naangusha machozi ya uchungu, nilihudhunika sana niliona sasa majukumu yananizidia, mtoto mdogo naanza kumiliki uchawi mkubwa kiasi hicho si laana kabisa hizi.
Shiiiit...!
Niliweka pembeni Hirizi ile kitandani kisha nilijifunga kitenge nikavaa na tisheti nikatoka chumbani nikaenda chooni nilivyotoka nikapita ukumbini nichukue kikali ili ninywe nilewe sana labda ndiyo nitapata usingizi kwani nisingeweza kulala na msongo ule mkubwa wa mawazo niliokumbwa nao.
Ajabu kuingia ukumbini nilivyotupa jicho tulipoketi mwanzo na Jr nilishituka kuona bado ameketi palepale huku kichwa akiwa kalaza upande kana kwamba amesinzia palepale.
Uvumilivu ukanishinda ilibidi nimsogelee ili nimwamshe akalale labda kazidiwa pombe.
Nilifika mpaka pale, kwanza nilipigwa na butwaa baada ya kukuta mezani kuna K-vant kubwa na ipo nusu!
“Pombe kali kwangu ni castle lite.”
Nilikumbuka maneno hayo saa hiyo nikiitizama ile K-vant ambayo bila shaka ilinyweeka bila hata kipoozeo kwani pembeni sikuona chupa nyingine zaidi ya pombe kali na glasi pembeni ambapo nayo ilikuwa nusu.
“We Jr!...”
Nilimwamsha kwa kumtikisa akashituka akafumbua macho huku akiyumba tu kitini.
“We vipi?”
“Poa.”
Alijibu, nikagundua pia sauti yake imebadika sababu ya kulewa kupita kiasi.
Nikaona kujibizana nae isingekuwa suluhisho ilibidi nimuite mhudumu, pale nililipia chumba kisha waliitwa walinzi wa bar hiyo wakaja kumtoa wakampeleka chumbani na pombe yake.
Nami nikaenda mpaka kaunta nikanunua konyagi ndogo na grand Malta moja kubwa nikaondoka ili nirudi chumbani.
Kwa mara nyingine tena wakati naondoka nilitupa macho mahali tulipokuwa tumeketi na Jr!
Nilichokiona kilinifanya nisite hata kutembea nikasimama na kukaza macho mahali pale huku nisiamini ninachokiona!

Sehemu 22 Sehemu 24
0
0