Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Dunia Ya Pili - 05

Purukushani za baba mkwe zilinichanganya kwa kiasi cha kutosha, ukichangia na mayowe ya watu mtaani ndo ikawa kabisaa!
Nikapagawa…
Taswira ya mimi nikiwa nyuma ya nondo ikajijenga akili mwangu!
Wee saa ngapi nisifanye tukio?
Akili ilifanya kazi haraka kama kompyuta, wazo la kukimbia likanijia akilini.
Kwa kasi ya ajabu nilichukua kitenge nikajifunga kifuani, nikachukua na prova nikalitupia mwilini.
Papo hapo niligeuka kwa kasi ya mwewe niliurukia mrango ule ambao haukuwa imara niliupiga teke ukafungukia nje! Mara nikasikia yowe!
“Mwiziiiiiiiiii… Jamani mwiziiii msaaada ukuu jamaniiii.”
Alikuwa ni baba mkwe kumbe tayari alishakaribia mlangoni kwetu, sasa kitendo cha mimi kuupiga mlango teke hadi ukafungukia nje ulimkuta akiwa karibu ukambonda ndiyo maana aliachia yowe!
Yowe ambalo kwangu lilikuwa sumu kabisa nilizidi kutimua mbio kali huku nikienda nisipopajua, lakini tayari wakati ule watu walishakaribia na kuniona hivyo wakaunga na mimi huku wakituma kundi la mbwa kunifukuzia.
Muda mfupi tu nikaona kundi la mbwa limeshanizingira huku mbwa hao wakibweka balaa!
Mara watu nao hao wakija na marungu, mapanga, mikuki na silaha mbalimbali tochi nazo zikasambaa eneo lile na kusababisha giza kupotea!
Nilichanganyikiwa, nikashikwa na kiroho cha uoga, kukimbia nilishindwa kwani kundi la mbwa lilishanizingira nikakosa njia.
Nilijikuta nikipiga yowe kali.

“Aaaaaaaahhhhhh!”

“Tulia Leylah upo katika ulimwengu wenye nguvu kubwa sana hahahaha! Hakuna awezae kukufanya chochote hata kwa kosa la aina gani, hahaha!”
Aliongea kiumbe ambae sikuwahi kumtambua hata kwa jina licha ya kwamba haikuwa mara yangu ya kwanza kuonana nae.
Kwanza sikujua ilikuwaje nikawa pale wakati muda huohuo nilikuwa kati kati ya mkasa mkubwa na wa kutisha tena mkasa uogopeshao mara mia hata ya uwepo wa simba mwitu.
Nilitulia kwanza nikajitizama kwanza, kisha nilitazama kushoto na kulia.
“Mmh!”
Niliguna kimoyo moyo, nikameza mate mepesi ya uoga.
“Siku zote nilishakwambia uache uoga wewe!”
Aliongea yule kiumbe huku akinisogelea na kunipiga begani, nilishituka mno sababu kiganja cha kiumbe yule kilikuwa kigumu kama chuma.
“Acha uoga!”
“Kwani wewe nani?”
Nilijikuta nimeuliza swali lile japo siyo kwa hiari ni kama nilishitukiziwa tu nikalopoka.
“Hahaha! Mimi naitwa Sauli ila wote hupendelea kuniita kifupi yaani Soul, wazungu wananiita “Giant of second world!” Hahaha!”
“Giant of second world ndo nini?”
Niliuliza.
“Kwa kiswahili tafsiri yake ni mbabe wa dunia ya pili.”
“Dunia ya pili? Kwani kuna dunia nyingine?”
Niliuliza.
“Yaa! Dunia ya pili ni ulimwengu wenye nguvu kubwa sana kuliko hata dunia unayoishi wewe.”
Nilishituka!
“Kwanini?”
Niliuliza.
“Utajua tu… Halafu ukiamua kuutumikia ulimwengu huu basi na wewe utakuwa na nguvu kubwa sana! Utakuwa juu ya viumbe wote huko duniani, kila kitakachokuwa kibaya kwako kitageuka mara moja kuwa historia ya miaka elfu moja iliyopita, naamanisha kila kitakachokuwa kibaya kwako kitasahaulika muda huohuo kwenye vichwa vya watu na kitapuuziwa haraka sana nawe utaendelea na mambo yako!”
“Hata nikiua?”
Nilijikuta nimeropoka swali ambalo lilinishtua hata mimi.
“Naaam! Naam… Utaua tu! Halafu marehemu ataonekana ndiye mwenye kosa hata wengi wakashangilia kifo chake.”
Aliongea kiumbe yule maneno ambayo yalinifanya nishangae mara tatu tatu.
“Usishangae bali unapaswa kutambua kuwa kwenye dunia yenu kuna uonezi mwingi mno! Mbaya zaidi sheria hazifuatwi badala yake makosa hufukiwa na pesa! Wenye pesa hutesa wasio na pesa na sheria haziwaangalii na hata pale mnyonge anapoamua kujichukulia sheria mkononi basi mambo humgeukia anaonekana mbaya mara mia zaidi ya aliekuwa akimnyanyasa.”
Aliongea kiumbe yule kisha aliweka kituo.
Nami nilimeza mate.
“Sitoongea mengi, ila subili nitamtuma mwanangu aje kwako utakuwa naye ana cha kuzungumza na wewe halafu utarejea kwenu ukiwa na maelekezo.”
Aliongea hivyo kiumbe huyo, mara alipohitimisha nilisikia sauti kama inajongea hivi nyuma yangu nilivyogeuka sikuona kitu, hata nilipogeuka mbele yangu yule kiumbe nae hakuwepo!
“Haaaaa!”
Nilihamaki.

“Vipi?”
Mara nilisikia sauti ya kijana pembeni yangu.
Kugeuka nilishituka kuona uwepo wa yule kijana handsome alienikabidhi jiwe la dhahabu siku kadhaa zilizopita.
“Mambo Leylah.”
Alinisalimia.
“Poa.”
Nilijibu kifupi sababu ya uoga mwingi niliokuwa nao.
“Ok, mimi mzima… Naitwa Samwel yaani Sam kwa kifupi.”
“Sawa mimi pia mzima, nashukuru kulijua jina lako.”
Nilijibu.
“Sawa karibu nyumbani Leylah jiskie huru kabisa sawa ee… Karibu.”
Yule Sam aliongea saa hiyo akinisogelea akanishika mkono, mwili mzima ukasisimka hata nywele, hii ilimaanisha yule hakuwa binadamu bali alikuwa ni kiumbe fulani wa kutisha aliejivika umbile la kibinadamu.
Muda huo nilishangaa tunatokezea kwenye barabara nzuri na kubwa ya lami, huku magari kadhaa yaliendelea kupishana.
Sisi tukiwa tumeshikana mikono, tulipita saiti yetu tulitembelea mpaka tukafikia shehemu yenye mkusanyiko wa majumba na watu wengi tu, eneo lile lilikuwa ni eneo la starehe kwani kulikuwa na miziki kila sehemu halafu eneo lile watu wengi walionekana wamelewa kwani ongea na matendo yao yalidhirisha wazi walikuwa wamelewa.

Sam akaniingiza sehemu moja ambapo palikuwepo na duka kubwa la nguo, hapo alinipa uhuru wa kuchagua nguo zozote nizipendazo, kweli nilichagua viwalo safi vya kisasa, viatu pamoja na manukato yenye harufu nzuri na tamu puani.
Sam akalipa shilingi laki nne na vichenji huku hela hiyo kwake ikionekana kama kachapua elfu mbili tu kwenye laki.
Kiufupi yule mtu alikuwa na hela nyingi mno!
Basi tukatoka hapo tukaelekea sehemu palipokuwa na duka la simu.
“Chagua simu nzuri hapo.”
Aliongea Sam.
Haraka haraka nikachagua Infinix hot 10 huku nikijihakikishia nimechagua simu nzuri mno na ya kisasa kwelikweli!
Sam alicheka!
Nikamshangaa huku nikijishitukia kuwa huenda nimechagua simu ya bei kubwa!
“Acha ushamba wewe hata hujachagua simu ya bei kubwa hiyo!… Chagua simu wewe!”
Aliongea nikabaki nimeduwaa nilimuangalia, kwanza nilijiuliza mbona ameyajibu mawazo yangu kagunduaje nilichowaza?
“Siyo hivyo Leylah sijagundua au huwezi kuchagua nikusaidie? Samahani kaka mkubwa hapo, naomba mpe huyu dada hako ka—apple ka milioni saba kalikotoka juzi kati hapa.”
Nilipigwa na butwaa hadi mgongo ulilia traasa!
“Usiogope Leylah chukua simu hiyo… Kaka mpe na hiyo fast charger ya elfu hamsini.”
Aliongea Sam kisha alitoa kitita na kumkabidhi muuza simu yule kisha tuliondoka huku nikiitizama simu ile toleo jipya kabisa la apple ambayo Afrika ilikuwa haijafika kabisa labda kwa nchi kama Marekani ndiyo zilikuwepo.

Tulivyotoka hapo tukaenda sehemu moja ambayo ilikuwa ni Lodge/Bar huko Sam alilipia shilingi milioni nne hela ambayo ingetuwezesha kuishi hapo ndani ya siku nne, kwa maana hiyo bar kwa siku moja mtu analipa milioni moja atalala atakunywa na atakula mapaka anakimbia ila kiingilio ni milioni moja kwa saa 24.
Basi baada ya Sam kulipia tulioneshwa chumba chenye hadhi yake, huko tulioga kwa zamu kisha nikajitupia viwalo vyangu, nikajipulizia unyunyu wangu wa bei kali baadae Sam nae alitoka kuoga akabadilika kisha wote kwa pamoja tulitoka chumbani tukaingia ukumbini mahali palipo na starehe za kila aina.
Tulitafuta sehemu tukaketi, pembeni yangu kulikuwepo na saketi nikachomeka simu yangu ikaanza kuchajiwa.
Sam aliagiza mizinga saba ya wine pamoja Malta kubwa makopo matano kisha alinikaribisha, nilikataa pombe akaniambia anajua ndiyo maana aliagiza kinywaji laini Malta.
Basi glasi zikafika pale kila mtu akaanza kujimiminia kinywaji chake pale, tukaendelea kuburudika kwa kinywaji na mziki mnene ndani ya bar hiyo basi ikawa ni starehe kwa kwenda mbele.
Baadae Sam alinipa laini akaniambia niweke kwenye simu yangu, niliipokea na kuiweka nikashangaa mtandao wa Vodacom umesoma kwenye mnara, muda huohuo ukaingia ujumbe kwenye simu yangu, nilipofungua na kuusoma nilitabasamu baada ya kukutana na hongera ya kupewa GB 50 bure na mtandao wa Vodacom kama zawadi kwa mteja mpya.
Hee! Nilifurahi sana! Lakini furaha yangu ilikatika ghafla nilipokutana na kitu kingine kilichonishitua kidogo, laini ile ilikuwa na majina karibu ya watu wote niliokuwa nafahamiana nao akiwemo shangazi yangu Jemima.
Nilitaka kumuuliza Sam lakini akili ilipuuza haraka mno baada ya kuliona faili la WhatsApp kwenye simu yangu haraka nikazama WhatsApp yaani nikawa kama mwehu na simu vile.
Huko nikaingia status nikakuta shangazi ameposti umati wa watu wakiwa wamebeba jeneza, huku akiwa ameandika kwenye status hiyo,
“Ya dunia mengi pumzika kwa amani Meddy.”
Nilishituka sana! Koo lilikauka ghafla, ikabidi niokote glasi ya Malta nikaigugumia kwa fujo hadi ikaisha kisha nikaibamiza mezani, nikamimina Malta nyingine hadi glasi ikajaa lakini muda huo huo nikajikuta naanza kujihisi tofauti tena hali ile ilikuwa ikinijia haraka mno!
Nilipotulia na kujisikilizia nikagundua kinywaji nilichokunywa kwenye glasi ile ya mwisho kilikuwa kimechanganywa na pombe!
Nikahisi kabisa Sam alinichanganyia pombe kwenye glasi yangu pindi nilipokuwa bize na simu.
“Sam umen…”
Kabla sijamalizia sentesi yangu nilipigwa na butwaa kwa tukio lingine tena nililokutana nalo machoni pindi nimeinua uso wangu kumtizama Sam.
Siyo siri lile tukio liliniacha kinywa wazi huku moyo nao ukitawaliwa na kitete kisicho na mfano!

Sehemu 4 Sehemu 6
0
0