Dunia Ya Pili - 16
Ikawa yapata saa mbili na robo asubuhi.
Niligeuka taratibu macho yangu nikayaelekeza mahala lilipojengwa soko kuu la mkoa wa Iringa.
Kama ilivyokawaida kwa eneo lolote la kibiashara nyakati za asubuhi, ndivyo ilivyokuwa pia pale sokoni, watu walipishana huku na huko,
maneno, vijembe na matusi ndivyo vilivyokuwa vikisikika asubuhi ile pale sokoni.
Nilipita karibu huku nikiangalia kuona kama ningeona chochote cha kunipendeza machoni nikakinunua.
Nilimwona mama mmoja mwenye mtoto akitembeza ndizi kwenye ungo, macho na mwili wa mama huyu vilionesha ni kwa jinsi gani mama huyu alikuwa
amekata tamaa na maisha, cha kusikitisha zaidi mwanae alikuwa akilia mno hata sikujua mtoto yule alikuwa akililia nini.
Nilimsogelea mama huyu nikamwamkia.
“Mama shikamoo.”
“Marahaba binti yangu hujambo?”
Alijibu salamu yangu ingali macho yake yakizidisha umande.
Hata nikahisi huenda salamu yangu ilimzidishia majonzi moyoni mwake.
“Pole mama, pole na kazi.”
“Asante.”
Alijibu kifupi, nayo macho yake akayahamishia kando, mbali kabisa na uso wangu.
Nilimsogelea nikamuuliza.
“Kulikoni mama?”
“Mwanangu kama utakuwa na shilingi mia tano tu, naomba unisaidie mdogo wako apate chakula nawe Mungu atakubariki utapata mara tatu yake.”
Kufuatia maneno yale niligundua ni kwanini mtoto yule alikuwa analia.
Kumbe ilikuwa ni njaa.
Dah! Ama kwa hakika kuna watu wana maisha magumu.
Nami pasipo hata kuwaza nilingiza mkono kwenye mfuko wangu wa sketi upande wa kushoto nikatoa burungutu langu la hela, hela iliyokuwa katika bajeti ya
kuliwa tu, nikamtolea mama yule kiasi cha shilingi elfu hamsini nikamkabidhi.
“Itakusaidia mama yangu leo na hata kesho ikiwa utaitunza.”
“Siyo kunisaidia kwa njaa tu… Bali pesa hii kupitia nguvu za Mungu mkuu, Mungu muumba mbingu na nchi, Mungu aliye juu mbinguni ataibariki pesa hii na
nitaifanyia mambo makubwa sana, asante sana na Mungu akubariki sana.”
Yule mama alipokwisha kuongea hayo aliondoka zake huku akiendelea kumbembeleza mwanae aliekuwa akilia mgongoni.
Nami niliondoka zangu wakati huo pesa yangu nikiwa nimeihamishia mkobani, nikatembea kwa mguu kutoka soko kuu mpaka msikitini hapo nilipanda Bajaj
iliyonikimbiza mpaka Orofea mahali ilipo nyumba yangu niliyoinunua siku chache zilizopita.
Huko niliikagua nyumba yangu kila idara nilipoona ipo salama nilitoka na kuanza kutembea huku nisijue ni wapi nielekee asubuhi ile.
Nilikuja kutokea RC Mshindo barabarani, hapo nilisimamisha bajaji nikakwea bajaji iliyonikimbiza mpaka Mlandege mwisho wa lami, nikashuka hapo.
Nikipokwisha kushuka pale moja kwa moja niliekea Zebra club, kama ilivyo desturi yangu kufika huko nilitafuta chumba ambacho hakikuwa na watu wengi sana,
nilijongea huko nikaketi kitini.
Nae mhudumu akifika muda huohuo kunisikiliza.
“Niletee safari tano kubwa.”
Niliagiza, halafu pembeni walikuwapo vijana watatu waliokuwa wakicheza karata huku wakiwa na lita mbili ya pombe za kienyeji iliyokuwa nusu.
“Halafu na hao rafiki hapo wapatie ya shilingi elfu mbili.”
Niliongeza.
“Sawa.”
Alijibu.
Baadae bia zangu zilifika pamoja na glasi yake kisha akawapimia na wale vijana lita nne ya pombe akawasogezea pale, walishukuru sana.
“Dah! Dada umejuaje tulivyokuwa tee! Hapa duh Asante sana!”
Aliongea mmoja wapo.
“Ah! Msijali maisha ndiyo hayahaya tu… Ulichonacho kidogo kula na wenzio.”
Nilijibu.
“Pamoko… vipi karata zinakuchomoka?”
Mwingine akaja na swali hilo.
“Ndiyo.”
“Aisee tumsogezee bi mdasi apo tuungane nae kwenye gemu.”
Wakahamia kwenye meza yangu, karata zikachangwa upya mchezo unaendelea basi ikawa tangu walivyonishirikisha kwenye mchezo basi umiliki wa
mchezo ukahamia kwangu magoli yote yakawa yangu nikawafunga hadi nikawachambua kama mboga.
Ikiwa takribani dakika arobaini tangu nifike pale mara simu yangu ilipata kupigwa.
Ilikuwa zamu yangu kutupa karata lakini nilisitisha nikawambia wao waendelee kucheza mi niongee na simu kwanza.
Nilifungua mkoba nikatoa simu yangu kuangalia nikagundua mpigaji ni Erick, nikaipokea saa hiyo nikiwa nanyanyuka kitini na kuelekea nje.
“Hallo.”
“Ee! Leylah mambo.”
“Poa mzima?”
“Mie mzima haswa, hofu kwako.”
“Mi pia mzima kabisa wa afya nisie na shaka hata kwa unywele!”
“Vizuri sana… sasa ule mchakato ndiyo tunauandaa hapa nilikuwa nataka nikupe taarifa kuwa katika muvi tunayotarajia kuitoa wewe
utasimama kama mke wa mtu huku pia ukicheza kama dereva wa bosi fulani mwenye pesa zake!”
“Uuw! Sasa mimi na gari wapi na wapi jamani? Hata kuwasha tu sijawahi.”
“Hahaha! Usiwaze, sasa cha kufanya uje mapema ili tukufunze gari ujue nini? Siyo kazi kwani hautakuwa unaliendesha umbali mrefu kwani ni kwaajili ya kushuti tu.”
“Sawaa.”
Niliitikia huku nikiisikia furaha ikianza kuja kwa umbali.
“OK, jitahidi sasa kuwa mfuatiliaji wa muvi ili uanze kuwa mbinu bora za uigizaji kabla ya kazi husika.”
“Usiwaze Erick nimekuelewa vizuri sana sitakuangusha katika hilo.”
“Poa.”
Simu ilikatwa, nikarudi ndani kuendelea kunywa mitungi nilikuta wale vijana watatu bado wanaendelea kucheza karata inaonekana safari hii kila mtu alipata
goli kwani walikuwa wamechangamka sana kila mmoja alikuwa na sauti kinywani.
Lakini lita nne yao ilikuwa imeshuka kiasi fulani hivi.
Hapo kuna kitu nikisoma ndiyo maana nilivyorudi sikutaka kuungana nao tena kwenye karata niliwaambia wacheze wenyewe kwani mie kwa wakati ule nilikuwa bize kidogo.
“Mhudumu waongezee ya buku na mimi niongezee bia moja.”
Zilikuwa zimebaki tatu nikaongeza moja zikawa nne.
“Ila hela yangu hujanipa we dada? Unajua nakudai shilingi ngapi?”
“Hata ingekuwa elfu hamsini ningekupa bwana we si ulete pombe kwani kuna mtu ataagiza kama hana hela?”
“Aah! Nipe kwanza hela yangu.”
Yaani katika vitu alivyonikera yule dada ni hicho tu, hata bia zake niliona takataka.
Kwa hasira nilifungua zipu ya mkoba wangu nikatoa rundo lote karibu laki tano na chenji nikaziweka mezani.
“Chukua hela yako yote unayonidai hapo.”
Nilimwambia, akaogopa! Na kwa aibu alianza kutolea maelezo mara ooh! Nisamehe nimwahi kuzurumika kwa njia hiyo ndiyo maana nikaongea hivyo nisamehe bure.
Nikamwangaliaa kisha nikacheka tu kimoyo moyo, nilichukua zile pesa nikachomoa elfu ishirini nikamtushia mezani kisha zingine nikazirudusha kwenye mkoba
nikaufunga na zipu halafu nikaendelea kunywa pombe huku nikiperuzi mtandaoni na simu yangu janja.
Niliendelea kunywa bia zangu huku nikiperuzi mtandaoni mpaka pale chupa zote zilipobaki kavu.
Nilivyomaliza zile bia nilihisi njaa, likanijia wazo nitoke nikale.
Nilinyanyuka kitendo cha kusimama tu, nikaitwa.
“Aah bi mdasi ndiyo unasepa au?”
“Ndiyo.”
“Ah! Freshi kwahiyo unatuachaje mama la mama?”
“Kivipi yaani?”
“Kopo linakata hapa?”
“Kwahiyo?”
“Fanya mautundu tuendelee kuishi.”
“Siku nyingine omba siyo unaweka njia ndeeefu ya kihuni siku nyingine hutosaidiwa… Mwambie huyo mhudumu awape pombe.”
“Poa barida sana mwanetu… Oya we mama kiduku lete mitungi hiyo tunajua chenji ya huyu sister ipo kwako ipo.”
Nikatoka zangu, migahawani hapakuwa mbali kutoka sehemu ile nilifikia mgahawa mmoja huko niliagiza ugali samaki kwani ndiyo chakula nilichojiskia kula siku hiyo.
Nikahudumiwa kama nilivyohitaji, nikala na kushiba kisha niliondoka mgahawani.
Nayo ikawa saa tano na nusu asubuhi, hapo nikapata wazo niende Check pointi bar nikachukue chumba nilale kwanza maana nilianza kuhisi uchovu
mwingi pamoja na ulevi ndani yake.
Kitendo cha kushika barabara inayoelekea Check point bar kuna hisia ziliniambia kuwa nyuma kuna mtu ananifuatilia.
Unaweza pia kusoma: