Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Dunia Ya Pili - 28

Jr alitabasamu mwenyewe kisha alitoa jibu…
“Unajua hapa ni mjini?… Hivyo kuna ujambazi sio poa! Ndiyo maana mwenendo wa ile gari niliushitukia nilijua tu huenda wanakufuatilia wewe kwa sababu wewe ni mgeni, na ni kweli mwenendo wa gari ile uliashiria kabisa ilikuwa ikikulenga wewe!”
“Asante kwa kunijali nashukuru mno! Halafu hebu tule kwanza siyo vizuri kula huku tukiongea ongea.”
Nilimsimamisha kuongea lengo langu niupishe ubongo ufanye kazi juu ya taarifa ile.
Maneno ya Jr yakanifanya nihisi wenge kichwani, akili ilianza kuchanganyikana wasiwasi ulianza kunitawala moyoni, papo hapo niliyakumbuka maneno ya Skobe kuwa Damson Mbarangu siyo mtu wa mchezo mchezo, alikuwa ni chui aliejivika ngozi ya kondoo kama mchungaji lakini nyuma ya pazia Damson Mbarangu alikuwa ni kiumbe fulani katili mno!
Ni mfanyabiashara mkubwa sana wa madawa ya kulevya huku akitumia kanisa kama kivuli.
Damson Mbarangu kuua kwake ilikuwa ni sawa na kucheka na mpaka hapo alikwisha poteza vijana wengi sana wa mtaani ambao waliomba kazi kwake matokeo yake kazi ikawashinda, Damson Mbarangu hakuwahi kumuacha mtu huru kutoka katika genge lake, iwe kwa kushindwa kazi au kumdhuru.
Alifanya hivyo ili kujilinda zaidi ya mchezo huo mchafu wa kihuni aliokuwa akiuendesha.
Nikayakumbuka pia maneno kutoka katika mzimu wa ukoo wetu kuwa yule mtu ni hatari mno sana hivyo sikutakiwa kabisa kukurupuka katika hili.
Hapo nilitulia kwanza nikashusha pumzi.

Jr aliendelea kutupia minofu inaonekana huyu Jr ni mpenzi sana wa nyama.
“Inaonekana unapenda sana nyama ee?”
Niliamua kuingizia hili kukata ukimya ulioingia kati kati yetu.
“Saana! Robo ya maisha yangu yametawaliwa na misosi ya nyama!”
“Weee! Kwanini sasa?”
“Basii tu! Hata sijui kwanini ila ndiyo hivyo mimi na nyama ni fisi na mzoga!”
“Hahahahahaha! Dah! Umenichekesha ingali sikuwa nimetegemea kucheka.”
Tulikula tukamaliza tukaagiza bia kadha laini aina castle lite tukawa tunashushia msosi tuliokula.
“Hivi Jr unahisi hao waliokuwa wakinifatilia ni kina nani?”
Nilimuuliza wakati nikiwa nimeweka glasi mdomoni ingali jicho lipo kwake nilijaribu kumsoma usoni wakati atakakuwa anatoa jibu lake.
Huku akitua glasi yake mezani...
“Mmh! Kwa kweli sikuweza kuwafahamu isipokuwa tu hisia zangu ziliniambia wale jamaa hawakuwa wazuri kwako.”
Ilijibu huku akinitizama mezani kana kwamba alikuwa akitafakari kitu.
“Kwani we utakuwa ukienda Magomeni mara kwa mara?”
Aliuliza.
“Sana kwa kuwa nina kazi kule.”
“Ayaaa! Sasa kuwa makini sana hata hawa boda boda siyo wote ni wazuri wengine ni vibaka!”
“Mmmmh!”
“Kweli… Yaani hapo nikushauri tu pendelea kupanda daladala japo nazo kuna wakati zinachelewesha sababu ya foleni.”
Papo hapo kuna wazo lilinijia.
“Kwani Jr siwezi kupata dereva muanifu nitumie gari ya ofisi kwa muda ambao nitakuwa sijui maana nina mpango wa kuwa na reseni lakini sijawa dereva kikamilifu.”
“Hiyo ni kampuni au?”
Aliuliza huku akinigeukia kwa haraka.
“Ndiyo!”
“Weeee! Fanya kweli basi nipe shavu hilo Leylah”
“Unajua kuendesha gari vizuri lakini?”
“Ndiyo na leseni ninayo hii hapa.”
Alinionesha.
“Tatizo hapa mjini uchawi mwingi sana ndiyo maana si wengine tunaamua kuwa vibarua tu mtaani.”
Katika maelezo yake Jr kuna kitu nilijifunza machoni kwake hata hivyo sikutaka kutilia maanani, kuanzia hapo nilianza kupanga mkakati kichwani niwapigie simu wale madalali nifike ofisini kwao niweze kununua gari ya kutembelea niliamini kuwa na gari kungeendelea kunirahisishia sana mambo yangu ya kikazi.
“Basi usiwaze ngoja kesho nifanye mpango niombe gari ofisini ili uwe dereva wangu.”
“Usiwaze na wewe nitakufundisha hadi uive vizuri sana na uje kuwa dereva mmoja mtata hapa mjini.”
Ongea yake ilianza kuwa ya kipombe zaidi, nikajua enhee! Keshaanza kuwaka huyo.
“Usijali rafiki.”
Kuna namna alinitizama baada ya kusikia neno rafiki.
Mara akamuita mhudumu kisha akaagiza value!
Doh!
Value ilifika akajiminia akawa anakunywa huku anacheza cheza kitini.
Namimi si nikaitamani…
Pombe kali si ndiyo zangu mie?
Nikachukua chupa nami nikajimiminia!
Akaagiza nyingine tena kabla ya kwanza haijaisha!
Nako upande wa saa ikawa imetimia saa tatu kasorobo!

Star Bar pakazidi kuwaka dj akaendelea kusambaza burudani ya muziki mule ndani kwa usahihi kabisa hali iliyopelekea watu wapagawe mwanzo mwisho!
Tuliendelea kunywa...
Muda wa mwisho kuna kitu nilishituka lakini kutokana na kuzidiwa na pombe sikuweza kukifatilia, hata sijui nililewaje ghafla kiasi kile maana ilifika mahali kila nikijaribu kushindana na ulevi ndo kabisa nilizidi kuelemewa fahamu zikawa zinanikimbia kabisa! Doh!
Kwa mbaali saana nilisikia milio ya risasi mfululizo nilishituka lakini hata kufumbua macho vizuri nijue ni wapi risasi zinalia nilishindwa nikaishia tu kutapatapa huku na kule bila mafanikio yoyote.

Kelele za harakati asubuhi ndizo zilizonitoa usingizini, kitendo cha kelele kupenya masikioni tu! Nilifumbua macho kwa kasi puu!
Nikakutana na chumba kigeni huku mwanga mkali wa jua ukiwa umepenya mpaka ndani, butwaa nililopigwa nalo halikuwa na mfano ubaridi mkali ulipenya katikati ya uti wa mgongo kutoka chini hadi shingoni sambamba na mapigo ya moyo kwenda mbio wazo la kuwa nimebakwa liliitawala akili yangu hapo ndipo nikazidi kuchanganyikiwa kabisa.
Kugeuka upande wa pili wa kitandani nakuta mwanaume kalala pale kifua wazi, eee!
Nilivurugwa mara kumi yake niliamka kwa hasira bila kufikiri chochote nikaokota mkoba wangu uliokuwa chini nikafungua zipu na kutoa bastola kisha nikaikamata vyema nilipania kufanya tukio baya sana pale wazo la kufanyishwa mapenzi bila ridhaa yangu lilinikoroga mtima wangu niligeuka na bastola mzimamzima ila kabla sijafanya chochote nikakutana na mwili nikakumbatiwa kwa nguvu!
Hilo nalo likaniletea mshtuko nikajikuta nafyatua risasi kiholela bila mpangilio bahati nzuri ikawa bastola ile nilikuwa nimeifunga kiwambo hivyo risasi zilitoka kimyakimya.
“Leylah unataka kuniua?”
Aliongea Jr kwa masikitiko huku akiniachia na kuketi kitandani.
Nikabaki nimeganda kama sanamu.
“Dah! Hivi serious kweli Leylah ulipania kunitoa roho?… Shida nini sasa kukuokoa kwangu ndiyo kunigharimu?… Sawa asante.”
Jr aliongea kwa uchungu huku akiangusha machozi aliinuka kitandani akaokota t-shirt iliyokuwa kitandani akaivaa akaokota sweta lake na kulitupia begani alianza kuondoka huku akifuta machozi.
Nilimwahi nikamzui ili asondoke.
Alinisukuma nilipepesuka kama karatasi nikaenda kujigonga ukutani, hata hivyo nilimwahi nikamkumbatia kabla hajafungua mlango.
“Jr tafadhali sana nipo chini ya miguu yako ninaomba tuongee tafadhali sana niliongea.”
Mara machozi mengi yalianza kushuka ni kweli nilijikuta mkosefu sababu ya kukimbilia kuchukua maamuzi pasipo kufikiria.
Kila nilivyofikiria kuwa mpaka wakati huo tayari ningeshakuwa nimeua!
Nilijuta mno moyo uliuma sana!
Nilijiona ni mkosefu mkubwa sana nilizidi kumshikilia Jr asije kuondoka mule ndani kabla hatujayamaliza, Jr kuona nimeng’ang’ania aligeuka kwa hasira huku macho yake yakiwa yameiva kama nyanya, safari hii niliishuhudia hasira yake wazi wazi machoni pake.
“Leylah niachie!”
Aliongea kwa sauti nzito ya chini iliyotisha.
“Jr tafadhali sana usichukue maamuzi ya kipuuzi kama niliyoyachukua mimi… Tafadhali sana nilichukua maamuzi nikiwa katika hali ya tahadhari bila kujua nipo na nani, naomba sana unisamehe Jr tuliza jazba tuyajenge kumbuka kuna kitu tunahitaji kukijenga.”
Niliongea huku mashavu yangu yakiwa yameloa machozi.
Maneno yale yalifanya anigeukie na kunitizama usoni...

Sehemu 27 Sehemu 29
0
0