Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Dunia Ya Pili - 25

Nilipomsikiliza kwa makini niligundua yalikuwa ni mazungumzo ya kibiashara, na yule alikuwa ni dalali.
Na ikawa kama bahati vile alivyopita kidogo usawa wa dirisha la chumba nilichopanga alisimama.
“Ni gari kali ndugu yangu, yule mzungu alikuwa padre hapa nchini sasa mkataba wa kuishi Tanzania umeisha inatakiwa arudi kwao Italia sasa ndo hivyo katika vitu anauzwa ni hiyo gari rand lover ni gari nzuri kama zile wanaotembelea watalii nyikani!”
Nilisikia hivyo nikaendelea kusikiliza japo mzungumzaji wa upande wa pili sikuweza kumsikia.
“Aah! Sheh yule nikimpanga hata milioni mia anapokea, ni gari nzuri ndugu Benja nimekupa hii tarifa ukiwa wa kwanza nikitaka ukiichukua siku tunazurura hapa mjini na ndiga kali hadi vibwengu wa mji watupishe!”
Maongezi yalikuwa marefu baina ya mwanaume yule na upande wa pili lakini ilivyoonekana kulikosekana uelewano kwani baada ya maongezi mwanaume yule alitoa simu sikiono huku akitikisa kichwa.
Haraka nilifunua pazia lote nikafungua dirisha, lilikuwa ni dirisha la alminiamu, nikatokeza kichwa nje.
“Samahani kaka.”
Alishtuka akageuka kwa kasi iliyojaa wenge.
“Mimi?”
Aliuliza huku akionesha kidole kifuani.
“Ndiyo, zunguka ingia unisubili ukumbini.”
“Sawa.”

Haraka nilirudi chumbani nikavua nguo za kulalia nikajifunga taulo kisha nikachukua mswaki nikautia dawa, nikaelekea bafuni.
Huko nilipiga mswaki nikaoga vizuri kisha nikarudi chumbani, huko nikajipaka mafuta mwili mzima.
Nikafungua begi langu langu la nguo nikachagua pamba kali ya kutoka nayo siku hiyo!
Kuna suruali nzuri sana ya bluu ambayo ilikuwa inanishika vizuri kabisa, kwanza nikaanza nayo nikaivaa nikajiangalia nikaona yes! Inafaa!
Kuna tisheti nzuri sana ya njano isiyoiva iliyokuwa na ramani nyeusi ya Afrika kifuani, nikatupia hiyo!
Nikaona nazidi kutoka!
Nikaona mambo si ndiyo hayo?
Mguuni nikatupia raba nyekundu...
Mkononi nikavaa saa ndogo ya mshare, shingoni nikajipamba kwa mkufu mdogo wenye rangi ya gold, mkufu huu ulikuwa na kidani cha nembo ya ‘Apple’ hakika nilivyojitizama kwenye kioo niliona sasa nimetokelezea!
Bado nini hapo?
Nilichukua bastola yangu nikaisweka mkobani, nikachukua simu yangu nikaiwasha kisha nikaishika mkononi nikachukua hirizi ya urithi nikaiweka kwenye mkoba.
Nikaangalia kiasi cha pesa kilichopo mkobani niliona kinanitoosha kabisa kwa siku hiyo kuanza nacho.
Kabla ya kuondoka chumbani nilimpigia Sam nikamjulia hali tuliongea mengi kidogo nikamjulisha kuwa siku hiyo nilipanga kuonana na huyo Erick halafu kingine siku hiyo pia ningeanza kuiendesha ile harakati ya kumpoteza duniani mchungaji Damson Mbarangu.
Alichonisisitiza Sam ni kuniomba niwe makini kwa kila hatua kwani kazi niliyopewa haikuwa nyepesi kama ilivyokuwa inazungumzwa kinywani.
Nilimuahidi nitakuwa makini kwa kila hatua niipigayo.
Tulimalizana hivyo kisha nilikata simu lakini kabla sijairudisha mfukoni simu ya Erick iliingia.

“Hallo!”
“Mambo dada?”
“Poa mzima wewe?”
“Mimi mzima kabisa hofu kwako?”
“Mimi pia niko salama.”
“Sawa… Kwahiyo tutaonana muda gani?”
“Kwani ni wapi kwanza?”
“Sisi kazi yetu tunafanyia Magomeni.”
“Ok,nitakujulisha nikianza kuja?”
“Au utapotea nikufate?”
“Hapana usiwaze nitakupigia simu lakini kama ni Magomeni nitakuja kabisa mpaka hapo halafu tutawasiliana ni wapi uje unichukue.”
“Sawa, jitahidi kidogo maana leo tutaanza kwenda lokesheni kufanya mazoezi.”
“Sawa usijali.”
Simu ilikata, nikachukua funguo za chumba nikatoka na kufunga chumba changu, nikaondoka zangu mpaka ukumbini.
Nilimkuta yule mwanaume tayari keshafika na kaagiza safari anaendelea kunywa taratibu.
Alikuwa ni mwanaume wa umri kidogo hivyo nilipaswa kumwamkia.
“Shikamoo!”
“Ooh! Poa mzima mdada?”
Nilimtizama usoni, moyoni nikajisemea inamaana hakusikia nilivyomsalimia?
Hata hivyo nikampotezea.
“Safi tu!”
“Sawa karibu...”
Ukarimu ulikuwa mwingi mno! Nami taratibu nikavuta kiti nikaketi.
Muda mfupi baadae mhudumu alifika kunisikiliza.
“Niletee safari tano.”
Niliagiza.
Tukaendelea kuongea.
“Karibu kaka… aah! Ni mimi niliekuita, nilisikia kama unazungumza kuhusu biashara ya gari na kwa kuwa na mimi nina uhitaji nikaona si mbaya nikatupa karata yangu pengine ikawa bahati.”
Nilianza kufunguka.
Kabla hajajibu mhudumu alifika na vinywaji akavitenga mezani akaacha na open ya kufungulia kisha akaondoka zake.
Yule mwanaume kwanza alinitizama kwa jicho fulani lenye kadharau ndani yake.
“Unafikiri ni IST hiyo? Au noah? Ana tax?”
Aliniuliza maswali ya kijinga mno! Hadi nikamshusha hadhi.
“Kama hamna kaka yangu si uniambie tu? Au...”
“Gari nilizoziona mpaka sasa ni Scania 114, Toyota crown, halafu nina Hilux new model, pia nina Harrier pia kuna Land Rover hii ndugu yangu bei yake ni kigongo.”
“Hiyo Land Rover umeuza kabisa bei gani ukiachana na bei ya maongezi.”
“Hiyo ni mia na kumi nimeuza mia napokea.”
“Hicho ndicho nilichokuitia sasa, je? Gari ninaweza kuiona?”
“Ndiyo! Ukifika kwenye ofisi zetu unaweza kuiona na hata kuikagua unaweza kuikagua tunakuruhusu uje na fundi wako.”
“Sawa niachie namba ya ofisi nitafika ofisini muda wowote kuanzia hivi sasa.”
“Sawa.”

Yule dalali alinitajia namba ya ofisi kisha baadae alimalizia bia kwenye chupa akaaga na kuondoka akidai ana mizunguko mingi sana asubuhi hiyo.
Dakika mbili baadae tangu kuondoka dalali kuna mhudumu alipita karibu yangu nikamwita.
“Samani yule kijana niliekuwa nae jana hapa bado amelala?”
“Mbona ameondoka muda mrefu sana!”
Jibu la yule mhudumu lilinifanya nishituke hadi nikasizi, sikutegemea kuwa huyo Jr angeondoka pasipo kuonana na mimi.
“Lakini kuna bahasha aliiacha kaunta aliomba tukupe ukiamka.”
“Kailete.”
Nilijibu haraka.
Muda baadae bahasha ilifika mikononi mwangu, kwanza nikaikagua kwa nje haikuwa na maelezo yoyote.
Nikaona kuiangalia nje napoteza muda, nikafungua ndani kuna karatasi niliona nikaichomoa haraka ajabu licha ya kuikagua mbele na nyuma hakukuwa na andiko lolote!
Nikaduwaa!
Ilibidi niiweke mezani kisha nichungulie tena ndani ya bahasha nikaona karatasi nyingine ndogo nikaitoa kuangalia nikakuta nayo iko tupu!
Nikaachia tusi la nguoni, kidogo niitupe ile bahasha lakini nikaghairi nikajipa moyo niangalie kwa mara nyingine tena.
Kweli nilivochungulia kwa mara ya tatu niliona karasi ndogo ikiwa imekunjwa vyema, nikaitoa nilivyoikunjua nikaona namba za simu.
Ile karatasi nimaisweka mfukoni kisha nikainuka kitini, bia nilizonunua sikunywa hata moja niliomba nihifadhiwe kaunta ningekuja kuzinywa.
Niliondoka nikaenda majikoni huko niliagiza supu ya maana, nikainywea huko huko baada ya hapo nilitoka mpaka nje nikapanda daladala moja kwa moja mpaka Manzese.
Nikashukia nyuma kidogo ya daraja, hapo nilisimama kwanza nikatoa ile karatasi yenye namba za Jr nikaingiza zile namba kwenye simu kisha nikapiga.
Iliita mara mbili ikapokelewa.

“Halloow!”
Simu ilipokelewa katikati ya kelele nyingi na ngumu utafikiri watu hao walikuwa kwenye harakati za kupasua mawe!
“Jr…!”
“Oya!”
“Leylah hapa!”
“Sana!.. Wapi dada?”
“Nipo Manzese hapa darajani we upo wapi?”
“Aisee! Mi umeniacha huku huku Mbezi kuna harakati moja hivi naofanya.”
“Eeh!”
“Vipi?”
“Kwani utakuja saa ngapi?”
“Sasa sikia dada Ley, kuna bi mkubwa moja ivi yuko mitaa hivyo anaitwa ant Salla, ulizia uende hapo utulie nitakukuta hapo.”
“Si utachelewa wewe?”
“Siyo sana, kwa sababu najua nina mgeni sitakawia sana niamini basi.”
Kabla sijajibu mara nilisikia tusi.
“We k**mae msenge huu siyo muda wa kuongea na malaya!”
Nilikereka sana nilitamani kumwambia kitu Jr bahati mbaya simu ilikata, hata nilivyojaribu kupiga tena sikumpata hewani.
Nikaamua kupotezea tu, niliondoka nilipokuwepo nikatembea hatua kadhaa mbele nikakutana na mwanaume mmoja, tukasalimiana kisha nilimuuliza kwa ant, Salla ndiyo wapi?
“Unaiona hii njia? Nenda nayo hatua kadhaa mbele mkono wa kushoto kuna jengo lina bango kwa nje limeandikwa K.PUB, ingia ndiyo kwa ant, Salla hapo.”
Basi baada ya kupewa maelezo hayo moja kwa moja nilinyoosha sehemu husika bila hata kupotea.
Kweli nilifika hiyo sehemu.
Nilifika bwana!
Hiyo sehemu wanaita K.pub au kwa ant. Salla hii ni sehemu ya biashara ya vinywaji vya pombe lakini mbali na pombe pia humohumo ndani kuna eneo maalum la kupumzika ambapo upande huo ni mahususi kwa nyama choma, chipsi na madiko diko kibao na huko ndiko anakopatikana huyo ant Salla.

Kwa kuwa asubuhi ile sikujisia kunywa pombe nililazimika kujongea mahali zinapochomwa Chipsi na nyama huko niliagiza Chipsi nyama, nikahudumiwa nikaendelea kuzisasambua taratibu huku nikivuta muda kumsubiri Jr alieniahidi kuwa angenikuta mahala pale.
Muda uliyoyoma nikiwa pale hatimaye ilifika saa sita na nusu na Jr hakuonekana, wala simuni hakupatikana, nilianza kukereka.
Baadae nilikata shauri kuwa niondoke tu nikajitegenee mwenyewe kwani suala la kupata mwenyeji lilishaingia mdudu kama hivyo.
Lakini kabla sijainuka kuondoka Jr alitokea!
“Wewe nilishaanza kuondoka ujue?”
Niliongea.
“Tatizo una haraka mno, wakati kanisani kwenyewe wanaingia saa kumi dada yangu.”
Aliongea huku akipitiliza mpaka jikoni huko akarudi na sahani ikiwa imejaa Chipsi nyama.
Kwa jinsi alivyoonekana Jr alionekana wazi kabisa alitoka kufanya kazi za saidia fundi halafu alikuwa hajaoga bado hivyo mwili mzima ulichafuka kwa matope na simenti.
“Pole na kazi lakini.”
Nilimlegezea sauti akatabasamu wakati huo aliendelea kutupia Chipsi haraka haraka.
“Asante pole kwako pia nimekukawiza sana.”
“Wala haina shida.”
“Sema nini?… Usiwe na shaka kanisani muda wa ibada bado sana kwahiyo apa tunakula bata mpaka mida yenyewe au siyo?”
Niliishia kumtizama tu usoni... Halafu nilivyokumbuka nilivyomtupia pesa jana usiku halafu akaziterekeza dah! Sikumpatia jibu huyu mtu.
Tukiwa pale mara simu yangu iliita, kuitoa nikaona ni Erick amenitafuta.
“Hallo Erick.”
“Ndiyo dada habari.”
“Njema habari mwenyewe.”
“Safi... Niko Manzese hapa kuna harakati naifanya mara moja, nikitoka hapa nitakutafuta ili uniambie ni wapi nitawakuta.”
“Sawa dada.”
“Poa.”
Simu ilikatwa.
Jr aliendelea kula chips kwa pupa ilionesha ni kwa kiasi gani alikuwa na njaa.
“We Jr taratibu utakabwa bwana... Halafu hata karibu hamna! Hee halafu unakula umesimama vipi?”
“Aah! We bi mdashi ee?.. anti Salla!”
“Abeee!”
Aliitikia, akaja.
“Nakusikiliza baba.”
“Mpe huyu dada Chipsi nyama za kutosha!”
Alisema.
Nikamuwahi.
“Hapana bwana mi nimekula, asante Jr.”
Niliwaona jinsi bar medi humo ndani walivyonitolea macho kitendo cha kukataa ofa ya Chipsi, nikacheka kimoyo moyo.
Basi Jr alimaliza kula chips kisha aliomba nimsubili aende akaoge abadilike nao muda ungekuwa umewadia ili tuanze kusogea maeneo hayo.
“Poa usichelewe sana au ni mbali sana?”
“Hapana ni karibu.”
“Sawa.”

Jr aliondoka, ili nisiendelee kukaa bure mule ndani niliagiza Grand Malta nikaendelea kunywa nikipoteza muda kumsubili Jr.
Kuna wazo likanijia la kumpigia Sam make ni masaa mengi yamepita sijawasiliana nae.
Nikatoa simu ili nimtafute, kitendo cha kutoa lock ya simu moyo ulilipuka kwa nguvu! Nilishangaa kukutana na missed call karibu ishirini kutoka kwa Sam.
Nilishangaa hizi simu ziliingiaje bila mimi kusikia! Macho nikahamishia kwa haraka juu ya kioo cha simu kuona kama simu ilikuwa katika mfumo wa mtetemo au kimya yaani ‘silent?’
Dah! Nilizidi kushangaa kwani simu ilionesha wazi kabisa ipo kwenye mfumo wa sauti.
Mmh! Ilibidi niingie kwanza kwenye missed call hizo nione simu hizo zimepigwa mda gani?
Ajabu kabisa simu ya mwisho iliingia dakika kumi zilizopita hee! Nilipagawa!
Ikabidi nipige hapohapo huku kichwani nikianza kupangulia sentesi za kujitetea.
Kitendo cha kupiga simu tu! Ni kama niliingia kwenye ruya vile.

Nikajikuta sehemu ya tofauti ndani ya mitaa iliyotulia iliyo na watu wachache waliokatiza huku na kule nao walikuwa bize sana na shughuli zao.
Wengine walipita kabisa karibu yangu lakini hakuna aliyethubutu hata kusemezana nami licha mimi kuonekana ni mgeni mahala pale.
Kuna mama mmoja alipita karibu na mimi, nilipata wazo la kuongea nae lakini kabla hata sijamsalimia ghafla niliiona gari ya Sam ikifika na kusimama karibu yangu.
Sam alishuka akiwa ndani ya suti safi yenye rangi ya bluu.
Nilipigwa na butwaa nikashindwa hata kumlaki.
Alifika karibu yangu akavua miwani.
“Mambo!”
Alinisalimia huku akinipa mkono!
“Sam…!”
Nilijirusha kwake nikajichimbia kifuani kwake.
Alinikumbatia akanibusu mfululizo kichwani shingoni na hata baadhi ya sehemu zangu za mwili.
“Mbona hupokei simu zangu baby?”
Lilikuwa ni swali lake la kwanza kwangu.
“Yaani hata sijui nisemaje? Ujue sikusikia? Sasa sijui ilikuwaje au mawazo yalikuwa mbali?”
“Ok sasa Leylah huku umekuja kikazi sawa?”
“Ndiyo!”
“Utajiri mkubwa ujao uko mikononi mwako sasa ni chaguo lako ufanye kazi uwe tajiri au la!”
“Kwanini wasema hivyo?”
“Nasema hivyo nikiwa na maana hii hapa! Mfalme Lucifer ametoa agizo moja kwako ukilitimiza ameahidi kukupatia vito hamsini mchanganyiko wa dhahabu, almasi yaani kila aina ya madini thamani yake itakuwa si chini ya bilioni hamsini Leyla unakwenda kuwa bilionea mwingine mkubwa sana duniani! Je upo tayari?”
Nilishtuka!
Nikajiuliza kwani kuna kazi tofauti na iliyo mbele yangu?
“Ndiyo! Kuna kazi nyingine ukiachana na hiyo ambayo inaelekea kukamilika!”
Kwanza nilishangaa! Sam alijibu mawazo yangu.
Nilitamani nimuulize alijuaje mawazo yangu, nikajikuta nimesahau halafu akaniambia kuwa niwe makini sana nisichanganye kazi na mapenzi na akaniambia niko huru kumteka mwanaume yeyote kimapenzi ikiwa kuna maslahi yoyote kutoka kwake mbele ya kazi zangu!
Nilishuka nikajikuta ni kama natokea usingizi, nikamwona Jr kasimama mbele yangu huku akiwa ananishangaaa!
“Leylah unasinzia?… Ona sasa umemwaga grand Malta.”
“Dah! Kwani hii ni ndoto au?”
Nilijiuliza kimoyo moyo ghafla kwa mbali nikasikia watu wanacheka!

0
0