Dunia Ya Pili - 03 
Kitendo cha kuzinduka kutoka katika hali ile ya kutisha ambayo sikujua kama ni ndoto au kitu gani, nilizinduka huku moyo ukiwa unaenda mbio mno!
Macho yangu mara moja yalitua kwa Amina.
Kilio chake kiliniongezea mashaka mara dufu, nilijaribu kunyanyuka huku nikiwa nimeloa maji mwili mzima, lakini kabla hata sijanyanyuka nilikumbana na
maumivu makali sana eneo la kitovu maumuvu yaliyonifanya nitulie na kurudi chini tena.
Papo hapo nikakumbuka.
“Tulia mke wangu utajitonesha mshono!”
Nilipokumbuka neno hilo nilimkumbuka mwanangu, muda huohuo kumbukumbu zilimiminika kichwani mithili ya maji yatililikayo!
Nikakumbuka nilivyomuona mwanangu katika ndoto akiwa kwenye mazingira ya kutisha mno! Akiwa kashikiliwa na joka huku akilia!
Mwili mzima ulisisimka, nikamtizama Amina, kisha nilimtizama Meddy, sura zao zilinipa ujumbe wa msiba.
“Amina mwanangu hajafa nimemwona akiwa hai.”
Nilijikuta nimeongea kitu ambacho sikutarajia kukiongea kila mmoja aliyekuwepo pale akashtuka na kunitizama usoni.
Meddy kusikia hivyo akanisogelea na kunitizama usoni huku midomo yake ikitetemeka.
“Umesemaje mke wangu?”
Aliniuliza.
“Mtoto wetu hajafa ni mzima kabisa yupo dunia ya pili.”
Kwa mara ya pili nilijikuta nimeropoka kitu ambacho hata ningekamatwa na kutakiwa kulitolea ushahidi nisingeweza kutolea maelezo
ila nilishangaa wakati ule nilikuwa nikiongea kwa kurazimishwa na kitu fulani ambacho kilikuwa kikinishinikiza mimi kuongea hayo pasipo hiari yangu.
“Dunia ya pili?”
Aliuliza.
“Ndiyo!”
Nilijibu.
Waliokuwepo pale walibaki kunishangaa.
Amina alinisogelea na kunigusa kwenye paji la uso akaanza kuomba, aliomba na kukemea nguvu zote za giza mwilini mwangu
mwisho alitangaza kuachilia moto kwenye himaya zote za kishirikina juu ya maisha yangu.
“Ninaachilia moto ulao katika himaya zote za kishirikina juu ya maisha ya Leylah na ninatumia nguvu ya uhai kwa jina na damu ya Yesu katika maisha
yake shindwa! Sh….”
Kabla Amina hajamaliza hubili lake nilijikuta nikishikwa na kichefu chefu kikali mara nilihisi kizunguzungu cha ghafla nikashindwa kuona vema
ghafla nikajikuta nimesimama kando ya mto ule ule nilipokuwa awali.
Maji yaliendelea kutiririka kwa fujo katika eneo lile la kutaniko la mito miwili huku macho yangu yakishuhudia mawimbi ya kutisha yakiendelea kuzunguka
eneo hilo la makutaniko.
Macho yangu yakatua lilipokuwepo lile joka lililokuwa limemshikilia mwanangu, ghafla nilitumbua macho na kubaki nikiwa nimeduwaa kama sanamu pale
nilipoona mwanangu kabaki miguu tu mwili mzima ukiwa tayari umeshamezwa na nyoka huyo!
Nilitamani kupiga yowe la nguvu lakini sauti ikanisaliti kutoka, nikabaki natetemeka kwa hofu kubwa iliyochanganyika na hudhuni moyoni.
Nilishuhudia kwa macho yangu yote mawili miguu ya mwanangu ikipotelea kwenye mdomo wa yule nyoka, pale pale macho yalijaa machozi yakaanza kutililika
kupitia mashavuni, kifuani hatimae chini.
Moyo uliuma kwa kiasi ambacho sijawahi kuumia tangu nizaliwe, sauti tu ndiyo ilinisaliti kutoka kwani ingetoka yowe ambalo ningeliachilia lisingekuwa na mfano.
Baada ya tukio lile papo hapo mazingira yalibadilika kutoka yalivyokuwa yakionekana nikashangaa yakionekana upya yaani kwa taswira mpya.
Mbele yangu niliona milima kadhaa iliyoonekana ikiendelea kujibadilisha taratibu mionekano, wakati huo kushoto kwangu kwa mbali niliona majumba
kadhaa yaliyojikusanya pamoja, bila shaka ile ilikuwa ni ngome kwa jinsi ilivyokuwa ikionekana.
Niligeuka kulia kwangu huko macho yangu yalikutana na msitu mnene ulioanzia chini kisha ukipanda juu kwa mpangilio mzuri, yaani eneo lile kulikwepo
na bonde hivyo kutoka bondeni chini miti iliota kwa usawa mzuri kuelekea juu kwenye mwinuko.
Ndege kadhaa walionekana wakiruka huko na kule kwenye miti ya msitu huo.
Nilimeza mate ya uoga kisha nikageuka mgongoni kwangu, toba! Nilishituka hata nikatamani kupaa!
Kiumbe niliekutana nae mbele yangu alitisha!.
“Hahahaaha… Karibu sana Leylah katika ulimwengu huu, ulimwengu wenye nguvu kuliko kitu chochote!”
Aliongea kiumbe yule atishae mwenye muonekano wa mzimu!.
Sikujibu chochote zaidi ya kuishia kuganda kama barafu huku nikitizamana ana kwa ana na kiumbe yule.
Kila mara mwili ulikuwa ukisisimka kwa hofu na uoga mwingi, laiti ningelikuwa na uwezo wa kukimbia basi dakika nyingi nisingekuwepo hapo.
Yule kiumbe mwenye mwonekano wa binadamu wa kutisha (mzimu) aliendelea kujiongelesha.
“Karibu katika agano la zama… Agano la karne hii lilikuchagua wewe kuchukua nafasi ya aliekuwa bibi yako Bi. Nelia.”
Nilishituka kusikia jina hilo!
Ni kweli Nelia alikuwa bibi yangu mzaa baba ambaye alifariki ningali darasa la sita, bibi alifariki akiwa na umri wa miaka 77.
Historia mbaya kuhusu bibi yangu niliisikia siku nyingi mno, ingawa sikuwahi kuamini wala kufuatilia kujua chochote, lakini za chinichini
niliwahi kusikia kuwa katika mlolongo wa kuliendeleza agano lililowekwa na mababu zetu miaka mingi iliyopita.
Bibi yangu Nelia alirithi kiti cha umiliki wa ukuu katika agano hilo na ilisemekana aliua watoto wake wote wa kiume akiwemo baba aliacha wa kike wawili
tu ambao ni shangazi yangu Jemima na mwingine aliitwa Ruth, ambae yeye inasemekana alikimbilia makanisani na hakuwahi kuonekana tena.
Inasemekana Jemima alirithishwa sehemu ya agano hilo, hilo lilizungumzwa kila uchwao mtaani.
Sikuamini lakini siku hii nilijikuta nikiamini mimi mwenyewe tena kwa asilimia mia!
“Mtoto wako katolewa kafara kwa takwa la mkuu wetu, na wewe tutakurudisha duniani hivi punde mazishi ya mwanao yatakapokamilika!”
“Mwanangu amekufa? Amekufa na nini? Anazikwa? Anazikwaje ningali sipo nipo huku?”
Nilijikuta nikimporomoshea yule kiumbe maswali kama mvua.
“Yaah! Amekufa pole sana, na huwezi kuhudhuria mazishi yake. Sikiliza tukuambie hata wewe pia tutakuua iwapo utapingana na sisi lakini
ukienda sambamba na sisi tutakufanya utakuwa tajiri mkubwa, siyo tu Iringa bali nchi nzima na utaweza kufanya biashara na wafanyabishara
wakubwa duniani ukafahamika dunia nzima hahahaha!”
Aliongea yule kiumbe nikajikuta najawa na tamaa ya kidunia!
“Sikia! Utapewa hela nyingi sana, na pia tutakupa mwongozo wa kuzitumia ili ukawae bilionea ndani ya muda mfupi tu sawa?
Kingine achana na mwanaume yule ni fara tu, olewa na mwanaume wa saizi yako Leylah vipi? Mbona unauangusha ukoo wako?”
Sikutoa jibu nilitulia nikiendelea kukitizama kile kiumbe.
“Nisubili hapo nakuja.”
Yule kiumbe aliaga kisha aliondoka.
Mara muda huo huo nikashituka naitwa nyuma.
“Leylah”
“Abee!”
Niliitika huku nikigeuka, nilikutana na sura nyingine tena!
Alikuwa ni mwanaume kijana Handsome mno! Hadi aliogopesha kwa jinsi alivyokuwa na sura ya kuvutia utafikiri american black fulani hivi shombe shombe,
mwanaume huyu aliyekuwa amevalia nguo za gharama kiatu kikali, saa ya pesa nyingi huku akiwa kajipulizia marashi yenye harufu tamu puani.
Alinisalimia.
“Mambo.”
“Poa.”
Nilijibu kifupi, bado nikiendelea kumtizama kuanzia chini mpaka juu, kitu kilichompendezesha zaidi ni nywele alizokuwa nazo, hakika yule mwanaume
alibarikiwa kuwa na nywele nzuri mno! Kama mwarabu fulani vile.
“Baba amenituma nikupe huu mzigo, amesema ukifika kwenu upeleke benki utapata hela nyingi sana, basi utaanzia hapo sawa?”
Aliongea yule mwanaume saa hiyo akinikabidhi mfuko wa nailoni nyeusi.
Niliupokea ule mzigo bila hata kuangalia ni kitu gani, niliuvilingisha kwenye nguo kisha niliufunga vizuri kabisa.
Yule mwanaume alinipunguia mkomo kisha aliondoka zake na kupotelea mitini.
Muda huo huo niliitwa nyuma yangu kugeuka nilimuona shangazi, wifi yangu Amina mume wangu Meddy na watu wengine kadhaa wakiniita
huku wakija mbio kana kwamba wananifukuza.
“Simama wewe Leylah!”
Sauti ya shangazi ilikuwa juu sana! Wakati ambao bado nashangaa sielewi nini kinaendelea, nilishituka nikivamiwa na kuangushwa chini kisha
nikafungwa kamba mikononi.
Unaweza pia kusoma: