Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Dunia Ya Pili - 24

Kwa jinsi nilivyomwona Jr hali yake ya kimwili ilionesha ni mtu mwenye maisha magumu mno pale Dare es salaam kana kwamba isingekuwa rahisi yeye kuidharau pesa ambayo kwake ilikuwa ni kama kuokota dodo chini ya mnazi.
Licha ya kwamba na nilikuwa mtumiaji wa rafu kwenye pesa lakini isingekuwa rahisi kuiacha pesa ile shilingi elfu hamsini ikiwa imezagaa kwenye sakafu ya baa ikaokotwa na watu wengine baki tu.
Nilienda mpaka tulipokuwa tumeketi na Jr nikazikusanya pesa zile kisha niliondoka kuelekea chumbani kwangu.
Nikiwa chumbani kwangu naendelea kupata kikali nilianza kumuwaza Jr, huyu mbona nae simuelewi maana Dar ni mjini kuliko miji yote?
Nisijeingizwa mji mpya mie!
Niliendelea kujiwazia huku nikiendelea kujipatia kikali taratibu, saa hiyo ikiwa ni saa sita kasoro usiku.
Baadae kuna wazo lilinijia bila kupoteza muda nilichukua simu yangu nikawasha data kisha nikaingia kwenye Google maps huko nikaitafuta kwanza ramani ya Manzese, nikaipata nikaivuta vizuri kwenye kioo cha simu yangu nikaanza kuitizama kwa makini nikazisoma baadhi ya sehemu, nikazivuta baadhi ya barabara za mitaa na vichochoro vyake.
Baadae nililitafuta na kanisa la Damson Mbarangu.
Nikaliona.
Nilitamani kuruka kitandani kwa jinsi nilivyopatwa na furaha ya ajabu moyoni.
Nikiendelea kuisoma ramani ile kwa utaratibu, nikaendelea kuzifuatilia baadhi ya barabara kadhaa za mitaani na chocho nikajikuta nakuwa mwenyeji ghafla pale Manzese.

Baadae nilihisi kuelemewa na pombe mwili ukawa unahitaji kupumzika, lakini kabla ya kulala ilibidi nimtafute Sam kwanza hewani…
Lakini kabla sijapiga simu ya Skobe iliigia.
“Hallo!”
“Leylah! Mambo vipi mrembo?”
“Safi.”
“Mbona kinyonge, au kisa upo Dar?” “Ndiyo!… Kwani kufika Dar ni jambo dogo?”
“Sawa… Vipi lakini?”
“Safi tu… Mbona simu za usiku kwanini?”
“Niliona haujalala ndiyo maana nimekupigia.”
“Wee mchawi nini?”
“Hahaha! Inawezekana!”
“Bwana mi nahisi usingizi sasa hivi.”
“Poa lakini najua katika kazi yako unahitaji sana msaada halafu mtu wako wa karibu yuko bize safari hii lakini usijali nitakusaidia.”
Nilitulia! Sikuelewa anazungumzia nini ndiyo maana niliduwaa.
“Hivi Leylah nikuulize swali?”
“Uliza.”
“Unajua uhusiano uliopo kati yangu na Sam?”
“Hapana sijui.”
Nilijibu huku nikiwa na hamu kubwa sana ya kujua ni uhusiano gani uliopo kati yake na Sam mpenzi wangu.

“Ninatafutwa sana na jeshi la polisi lakini kamwe hawatoweza kunikamata tena milele! Kwa kuwa nina nguvu kubwa sawa na Sam, ndiyo maana wewe kama shemeji yangu niko radhi kukusaidia kwa kuwa jukumu ulilopewa kidogo limekuzidi nguvu kwani huyo mchungaji unaekwenda kupambana nae ana nguvu kubwa sana kimizimu kwahiyo ukienda vibaya utanyongwa mwenyewe!”
Nilishtuka!
Ni maneno ambayo sikuyategemea kwa wakati ule!
Kwanza hata pombe zilinitoka!
“Unamaanisha nini kusema hayo?”
Nilimuuliza.
“Ni hivi… lile kanisa linaendeshwa kwa nguvu kubwa ya kishirikina nguvu ambayo mchungaji huyo aliitoa huko Nigeria hivyo siyo wa mchezomchezo kama unavyomzania… Halafu kingine sasa usichokijua! Unaelekea kugonganisha nguvu tatu kwa wakati mmoja, ujue kifo chako kitakuwa kibaya sana!”
“Skobeeee!”
Nilipiga yowe mara nikatoka usingizini dah! Kumbe nilikuwa ndotoni.
Kwanza niliiokota simu yangu iliyokuwa pembeni nikaangalia kama kweli nilikuwa naongea na Skobe au?.
Ajabu kutoa lock ya simu niliona sehemu nipoishia mara ya mwisho ni pale nilipoifikia namba ya Sam lakini sikupiga.
Nilishangaa!
Mbaya zaidi muda huo ilikuwa yapata saa saba na nusu usiku.
“Ee kunaelekea kukucha halafu hata sijalala mie ee!”
Niliamua kuzima simu kisha nilichomeka chaji kisha niliipanda kitandani nikajifunika ili nilale.

Nilifunua shuka ghafla na kulitupia mbali huko!
Macho yalikutana na mwanga mkali wa jua nikafumba haraka, ilikuwa ni taharuki kubwa ya moyo sababu ya ndoto za ajabu nilizokuwa nimiziota usiku ule cha ajabu hakuna ndoto hata moja niliyoikumbuka isipokuwa nilikuwa nikikumbuka baadhi ya ndoto niliota nikiwa nafukuzwa na viumbe wa ajabu ajabu mara niliota nipo kati kati ya kundi la wachawi yaani mauza uza kama yote!
Hicho ndicho kilichopelekea nikurupuke kwa wenge pindi natoka usingizini.
“Hivi maisha gani yenyewe haya?”
Nilijiuliza huku nikiwa ndani ya tafakari nzito.
Kiukweli maisha niliyokuwa nikiyaishi kipindi hicho yalikuwa yanatisha hadi mimi kuna kipindi niliyaogopa.
Basi ikiwa yapata saa mbili na nusu asubuhi nilinyanyuka kitandani nikatembea mpaka dirishani mahali ulipokuwa unapita mwanga wa jua asubuhi ile.
Nilisimama pale zaidi ya dakika mbili na sekunde nikitizama nje, kama ilivyokawaida kwa sehemu zote zenye mikusanyiko ya watu ndivyo ilivyokuwa pia maeneo ya nje ya bar ile.
Mpishano wa watu ulikuwa ni mkubwa sana!
Kila mtu alikuwa bize na mishe mishe zake,watu walipishana kama nyuki mzingani, wenye biashara na wasio na biashara wote walionekana kukatiza huku na kule.
Mara alipita mwanaume mmoja karibu na bar hiyo upande wa nyuma mahali lilipokuwepo dirisha la chumba nilichopanga, mwanaume huyu alikuwa anaongea na simu.
Simu yake ilinifanya nimsikilize na kumtiza kwa makini...

0
0