Dunia Ya Pili - 14
Maneno yale yaliniacha na tafakari nzito ndani ya Mtima, nikajikuta najuta kwa maamuzi yangu nilihisi hata siku moja ningehukumiwa kwenda
motoni kwa sababu licha ya kukumbwa na jaribu lile, mimi mwenyewe nilifanya maamuzi ya moja kwa moja ya kukubaliana na jaribu lile sababu
ya tamaa ya pesa.
Hata hivyo sikuwa na jinsi tena, kama ni maji nilishakuwa nimeyavulia nguo hivyo sharti lilikuwa ni kuyaoga tu si vinginevyo.
Palepale tukaongea na yule mama tukayamaliza.
“Una akaunti ya benki yoyote?”
Aliniuliza.
“Hapana.”
Nilimjibu.
“Sawa nitakusaidia kufungua… Na vipi ungependa kutumia benki gani kati ya NMB, CRDB na nyinginezo?”
Aliniuliza.
“Ninapendezwa na benki mbili tu hapa nchini nazo ni hizo uliotangulia kuzitaja.”
“Kwahiyo hapo nikufungulie akaunti kwenye ipi kati ya hizo mbili?.”
“Mmh! Hapo tufanye NMB hiyo CRDB si mahususi kwa wafanyakazi hasa kwenye makampuni?”
“Hata siyo hivyo… Isipokuwa kama umeipenda NMB basi nitakufungulia akaunti NMB.”
“Sawa.”
Basi palepale madam Angelina aligeuza gari tukarudi na barabara ile kwa mwendo wa taratibu huku akishusha vioo vile vyeusi kisha vikabaki vile
vya kuangaza, akafika mpaka njia panda, hapo alisimamisha gari akatizama kushoto na kulia akaona hakuna chombo chochote cha moto kinachokuja.
Haraka alikanyaga mafuta huku akizungusha usukani kuingia barabarani, ghafla kuna boda alikuja spidi kama mshale akitokea round about kule,
papo hapo madam Angelina alikanyaga breki za ghafla hata gari ikasimama kwa kunesa, tayari bodaboda alishapita kitambo huku ndani yule madam akatukana
matusi ya nguoni huku akimtizama kwa macho ya husda pindi anapotelea bondeni.
Aliingia barabarani huku akiongea ongea.
“Hawa ndio huwa wanatuletea matatizo hawa.”
Akasonya.
“Ni kuwasamehe tu dada yangu wengine vilevi vinawakataa wanajikuta wanakuwa na matendo mabovu sana.”
“Ni kweli lakini kumbuka akikupalamia tayari kuna usumbufu.”
Wakati tunaongea hayo tayari tulikuwa tukilipita jengo la chuo cha VETA Mlandege.
Tukafika mpaka Mlandege lound about, hapo alifunga breki tukasimama sekunde mbili msongamano ukapungua kisha Madam alikanyaga mafuta tukaingia
kwenye high way tukawa tunashuka na mteremko wa kushukia Mshindo.
Mshindo tukapapita hatimae tukakaribia kuingia mjini,lakini mjini hatukufika tukapita barabara za mashariki ya mji, tukapita soko kuu la mkoa
huko tukaendelea na safari tukapita mitaa ya Gerezani, kisha hospitali ya rufaa, baadae tukaja kutokea jengo la SIASA NI KILIMO, huko tuliingia
ndani kisha madam alitafuta egesho zuri akaegesha gari yake.
“Leylah.”
“Abee.”
“Hapa tunaingia ofisi za NIDA, na hii ndiyo hatua ya mwanzo kabisa.”
“Sawa.”
Nilijibu sawa ingawa sikujua sasa tumefika pale kwa dhumuni lipi sasa.
Tulishuka garini tukanyoosha moja kwa mpaka ndani ya jengo huko tukaingia flame ambayo ni ofisi ya NIDA nako baada ya salamu madam alieleza shida yake.
Aliwaambia wafanyakazi wa pale kuwa mimi ni mwanae nina changamoto kubwa ya namba ya NIDA hiyo ilikuwa ni changamoto kubwa sana kwangu na kwake kwani
nilikuwa na changamoto kubwa sana ya kishule na ni changamoto iliyokuwa ikihitajika namba za kitambulisho hicho haraka sana iwezekanavyo tena siku
ifuatayo au ingewezekana siku hiyohiyo.
Wale wafanyakazi walipotaka kuleta maelezo yao nao haraka aliwazima na laki nne za harakaharaka wakatulia na kazi ikaanza upesi.
Lilikuwa ni swala la kufatilia karibu miezi minne au zaidi lakini kupitia nguvu ya pesa mambo yaliisha palepale nikapewa namba zangu na kuambiwa
kitambulisho chake nisubiri ndani ya wiki mbili kingekuwa kimekamilika wakachukua namba ya madam Angelina wakamwambia wangempigia pindi
kitambulisho kimekamilika.
Tukatoka na kuingia kwenye gari kisha tuliondoka hapo.
Napo tulikata mitaa kwa mitaa hata tukaja kutokea sheli ya HOPE iliyo karibu na TANESCO Iringa, hapo Madam Angelina alienda kuegesha gari yake
sheli kisha tulishuka tukatembea na kuvuka barabara na kuingia ndani ya jengo moja kuuubwa!
Ni moja kati ya majengo tishio ndani ya mji kwani ni jengo refu kwenda juu kama mnara kisha chini pia limejengwa kwa ustadi wa hali ya juu,
ndani ya jengo hilo pia kuna benki ya NMB.
Tukaingia humo, shida yetu kubwa ikiwa ni kufungua akaunti yangu ya benki.
Michakato haikuwa mingi sana iliyochukua takribani dakika kumi tu akaunti ikawa imekamilika, papo hapo madam alitoa simu yake akaibofya
bofya ndani ya dakika tano yuko bize mara nakasikia ujumbe umeingia kwenye simu yangu.
Kufungua nilipigwa na butwaa la ghafla baada ya kuona meseji ya uthibitisho kuwa nimepokea kiasi cha
Tshs 6,540,226 (Bilioni sita, laki tano na arobaini elfu, miambili ishirini na sita!) Kwenye akaunti yangu ya NMB.
Hakika nilihisi na mishipa ya damu imepanuka nayo damu ikaanza kutembea kwa fujo mwili mzima.
“Nimekuingizia bilioni sita na laki tano hapo.”
Aliongea Madam Angelina.
Nao wafanyakazi wa benki wakamtizama kwa kile alichokiongea madam kisha wakanitizama na mimi.
“Hela ya kula unayo au unatoa kiasi kidogo cha kula?”
Aliniuliza.
“Hapana madam hela ya kula ninayo.”
Nilijibu.
“Sawa tuondoke.”
Tukaodoka ndani ya benki tukatoka nje ya jengo lile kisha tulivuka barabara na kuingia sheli ya HOPE mahali tulipoegesha gari yetu.
Tuliingia ndani ya gari, madam akaisogeza gari yake sheli akaongeza mafuta kisha tukaondoka zetu kurudi Tembo bar.
Kuna wakati nilijiskia fahari sana kumiliki pesa lakini pia kuna muda niliyafikiria na majuto yake huko mbeleni kwa kuna msemo usemao
hakuna chenye faida kisicho na hasara hivyo kuwa na pesa kweli tayari nilishakuwa nazo lakini kiuhalisia kabisa pesa zilikuwa ni za shetani
pesa zilizopatikana kwa kafara ya roho za watu, pesa ambayo ni ya moto kuliko hata umasikini wenyewe!
Dah niliwaza sana pindi tunaelekea Tembo bar.
“Vipi Leylah mbona unawaza sana?”
Angelina alinigutusha na swali pindi nimezama kwenye kilindi cha mawazo.
“Hapana madam siwazi nipo kimya tu.”
“Kweli?”
“Ndiyo.”
Ni kama hakuamini vile, halafu nae alipotezea.
Tulifika tembo bar, huko madam aliegesha gari mahali alipolitoa mwanzo kisha tulishuka tukaingia tena bar.
Lakini tulipoowacha kina Sam hatukuwakuta na yule mama mwingine nae hakuwepo.
“Sam ameondoka?”
Nilijikuta nauliza kwa sauti kubwa halafu nisijue sasa namuuliza nani.
Nilitoa simu kwa lengo la kumpigia lakini yule mama aliniwahi na kunishika mkono.
“Kwani una shida nae kubwa?”
Aliniuliza.
“Wala.”
“Basi utulie atarudi tu hajatoka mbona gari yake ipo nje kwani hukuiona?”
Alivyosema vile papo hapo nilikumbuka ni kweli land Rover ya Sam niliiona nje karibu mara mbili ingawa akili haikukumbuka kuwa ile gari ni ya
Sam licha ya kuwa nilishamuona nayo na nikapanda kabisa.
Niliposikia na kukumbuka kuwa gari yake ipo nje, nikapotezea nikawa na amani.
Mama yule aliagiza tena dompo tano za maana na glasi zake.
“Kunywa pombe mdogo wangu… Maisha yenyewe ni mafupi sana haya usipofurahi leo utaja furahi ukiwa kaburini?”
Mie niliishia kutabasamu tu.
Tulianza kunywa zile pombe, mara muda si mrefu nikimwona Sam akija akitokea vyumbani huku akijiweka weka shati yake vizuri.
Moyo wangu ulilia tusu nikahisi kabisa Sam anatoka kulala na mwanamke.
“Sam amenisaliti.”
Nikaongea kimoyomoyo huku nikimtizama kwa kumkazia macho kwa mbali.
“Hakuna wewe mie sijakusaliti tena futa kabisa hayo mawazo.”
Kitu cha ajabu kabisa Sam aliyajibu mawazo yangu wakati niliongea kimoyo moyo yeye akanijibu kwa sauti kana kwamba aliyasikia mawazo yangu!
Sasa cha ajabu kabisa ni kwamba licha ya Sam kujibu kwa sauti huwezi kuamini sauti yake ni mimi tu ndiye niliyeisikia!
Aliongelea umbali wa mita tano, lakini sauti yake ilisikikia ndani ya masikio yangu kana kwamba aliniongelea masikioni,
nilipigwa na butwaa nikamgeukia Madam Angelina nilihisi huenda alisikia!
Ye ndiyo kwaanza nilikuta yupo bize na simu.
Mmh!
Sasa nilipogeuka kumtizama Sam, nikashituka tena kwa mara ya pili baada ya kuona yule mama tuliemwacha na Sam nae akitokea kulekule alikotoka
Sam huku akionekana kulegea sana mwili hata macho yake akawa anatizama kwa kulembua!
“Mmh! Hawa si walikuwa wanafanya mapenzi hawa?”
Nilijiuliza kimoyomoyo.
“Hapana nimekukatalia Leylah mbona unawaza tofauti wewe?”
Kwa mara ya pili tena sauti ile ilisikika masikioni mwangu huku mwongeaji akiwa bado yupo umbali uleule tena akicheza cheza muziki kabisa!
Nilishangaa!
Siyo kushangaa tu! Hata kuogopa pia niliogopa tena sana maana alichokuwa akinifanyia Sam kilikuwa si kitu cha kawaida kiliniduwaza mno!
“Vipi Leylah kwani una tatizo?”
Alinihoji yule mama Angelina, niligutuka nikamgeukia nikagongana nae macho akinitizama kwa mshangao mkubwa huku simu yake akiwa kaitua mezani.
“Ah! Huyo nae ana vistress vya ajabuajabu hata ananiboa wakati mwingine.”
Kabla sijajibu Sam alijibu huku akipita mezani akanyanyua chupa moja ya dompo akawa amesimama staili ya miondoko.
Yule mama akabaki anatushangaa tu.
Kweli Sam aliondoka huku akiwa kashika chupa ya pombe mkononi, nilishindwa kumwelewa! Halafu cha ajabu sasa! Yule mama wa pili aliebaki na
Sam mwanzo hata nikawatilia shaka kuwa huenda walienda kufanya ngono nae alipotea mule bar katika namna ambayo sikuelewa.
Hakuwepo tena!
Licha ya kuangaza macho upesi huku na kule bado sikumuona!.
Pale nilinyanyuka kumfuata Sam, mara ya mwisho nilimuona mlango wa kutokea nje! Ile nafikia mlangoni nilimuona tayari yupo kwenye gari anafunga mkanda.
“Khaa!… Huyu mtu kafikaje kwenye maegesho mara hii?”
Nilitahamaki.
“We mbona kila kitu unashangaa shangaa tu vipi?”
Niliisikia sauti ya Sam ikiongea nyuma yangu! Kugeuka nikashangaa ni mtu mwingine tofauti nae alikuwa akiongea na mtu mwingine huku wote wakiwa
wameshika pombe mikononi mwao!
Mmh!
Kugeuka mbele naona Sam anageuza gari akiwa tayari kuondoka.
Nilikimbia hadi nikamfikia.
“Sam simama tuongee tafadhali.”
Sam alisimamisha gari akaniangaliaaa! Wakati huo alishajifunga mkanda na machoni alishavaa miwani miyeusi.
Akafungua mkanda akashuka kwenye gari…
Akavua miwani yake kisha akanitizama usoni na macho yake yaliyobadilika kulingana roho yake ilivyokuwa kwa muda ule.
“Nakusikiliza.”
Aliongea.
“Sam mbona unanifanyia haya? Au kwa sababu moyo wangu umekuwa dhaifu kwako kwa sababu ya kukupenda?”
Nilianza kushusha mistari, cha kushangaza Sam alicheka kwa dharau.
“Umeanza dharau siyo?… Hivi nyie wanaume mpoje?”
Niliongea kwa hasira huku nikimtizama kwa macho makali.
“Shika hii vaa kisha nitizame mimi, itizame gari yangu kisha litizame hilo jengo unaloliona halafu uniambie kama unanipenda au unanijaribu?”
Alinipa miwani huku akiwa kanikazia macho, nami nikaipokea haraka na kuivaa!
Toobaa! Nilitamani kupiga yowe la ukunga!
Nilivyokuwa nikiviona kwa macho ya kawaida niliviona tofauti tena kwa taswira ya kutisha!
Egesho zima la magari, hakukuwa na magari tena bali yalikuwa ni mauza uza ya ajabu kabisa mfano gari la Sam lilikuwa ni Jeneza kubwa sana la shaba,
gari la Angelina lilikuwa ni limnyama fulani la kutisha mfano wa farasi si farasi yaani sijui ni limnyama gani tena lilikuwa na pembe
pamoja na meno yaliyotokeza nje!
Hakika kilikuwa ni kituko chenye kuogopesha mno!
Hata yale magari yaliyosalia nayo hayakuwa magari, zingine zilikuwa fisi, zingine zilikuwa punda, vipembe, nyungo, na usafiri
mwingine tofautitofauti wa kichawi.
Nilishusha pumzi kisha nikageuka kumtizama nae Sam!
Mamaaa!
Nilitamani kukimbia nipotee kabisa eneo lile nisionekane hata ukucha!
Sam alifanana na Zombi, mwili wake ulikuwa umeoza huku ukitoa funza japo alionekana kuwa hai sababu kujihimili mwenyewe kwa kusimama na pia
viungo vyake vilikuwa vinafanya kazi, ila cha kushangaza zaidi ni pale kila kiumbe kilichocheza tu! Madonda ya sehemu hiyo yaliangusha
funza walioshiba ardhini.
Sam niliachana nae! Nikageukia bar!
Huko nako nilikutana na kituko cha mwaka!
Lile jengo zuri nililoliona mwanzo hata halikuwa hilo!
Baadala yake niliona jengo kubwa sana lililojengwa kwa mfano wa kaburi huku mbele likiwa na mlango, mlango usio hata na geti ambao ndio watu walio
kuwa wakiutumia kuingia na kutoka, halafu juu jego hilo lilikuwa na msalaba uliokaa upande, kisha pembeni ya msalaba huo kulikuwa na mfano wa
mkono wa mfu uliochomoza kutoka kwenye jengo hilo!
Muda huohuo Sam alinivua miwani ile, kitendo cha kuvulia tu miwani ile nikakuta kila kitu sasa linaonekana kama mwanzo.
Nikazidi kushangaa.
“Usipende kufuatilia vitu visivyokuhusu mke wangu kwanini lakini?… Unanikera sana! Sasa ngoja nikuambie mimi ni mfu mtarajiwa sawa?
Mwili wangu utakavomalizikia kuoza nami nitakufa huku duniani kwa kifo cha kumshangaza kila mmoja ingawa sitakuwa nimekufa kwani nafsi
yangu bado itakuwa hai, sasa nakushangaa unavyodai ya kuwa unanipenda! Je Bado unanipenda?”
Aliniuliza huku akinitizama usoni.
Nilikosa la kumjibu, wakati huo mwili bado ulikuwa umekufa ganzi kwa lile uzauza la kutisha nililopata kulishuhudia.
Unaweza pia kusoma: