Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Dunia Ya Pili - 18

Hatua kadhaa nilikutana na Sam, humohumo ndani inamaana nae alikuwepo isipokuwa hatukuwa tumeonana.
Nilimsogelea na kumsalimia.
“Vipi Sam.”
“Safi, vipi ndiyo unaondoka?”
“Niondoke niende wapi sasa?… Afadhali hata nimekukona.”
“Mimi hapa sasa!”
Aliongea huku akioneshea kidole chake cha shahada kifuani.
“Aah! Sasa una ratiba gani hapa jamani.”
“Si tunaenda zetu Leopard au?”
“Aa wewe… Sitaki mimi.”
“Kwanini?”
Aliniuliza ilihali akinitizama kwa usoni kwa jicho la tabasamu.
“Sitaki pombe sasa hivi sina hamu nazo.”
“Aaah! Kwani ukienda bar ni lazima unywe pombe?… La hasha! Kuna vinywaji laini kama vile Malta, komfuu led bull, soda na kadhalika.”
Aliongea huku akionesha tabasamu la kufurahi ilimradi tu anishawishi.
“Ili nikiwa na Malta uniwekee pombe zako kwenye kinywaji changu, unafikiri sikufahamu wewe?”
“Siyo kweli bwana hebu twende au twende hotelini?”
“Angalau hotelini.”
“Sawa twende kuna hoteli moja iko hapa mjini nafikiri hujawahi kufika.”
Tulitoka mule ndani ya ngome mpaka nje huko tukanyoosha moja kwa moja sehemu ya maegesho.
Kama kawaida Sam alikuwa na gari yake ileile ya kibabe land Rover toleo jipya kabisa.
Tuliingia kwenye gari akalitia moto tukaanza kuondoka taratibu huku nikiyaangaza macho yangu huku na kule! Kwa mara ya pili niliuona ule msukule wa Meddy.
“Haaa! Sam.”
Nilitahamaki nikamwita.
“Vipi?”
Aliuliza pasipo kunigeukia licha ya kumwita kwa tahamaki kubwa.
“Nimemuona Meddy.”
“Yuko wapi?”
“Si yule…”
Ooh mara asionekane nikabaki nimeduwaa.
“Alikuwa pale nimemuona kweli alikuwa pale.”
Nikaanza kutetea hoja yangu pasipo ushahidi.
“Hivi ujue Leylah kuna wakati huwa unanishangaza sana! Hahahaha!”
Sam alicheka hadi nikashangaa.
“Sasa unacheka nini?”
“Umeona mawenge bwana.”
“Mawenge?!”
“Yuko wapi sasa?”
“Duh…”
Nilikosa namna ya kuongea nikaonekana mzushi hata nikachekwa.Niliamua kutulia tu na kukubali kuwa niliona malienge basi ingawa moyoni nilibaki na msimamo wangu uleule kuwa niliuona msukule wa Meddy tena ile ilikuwa ni mara ya pili.

Safari haikuwa ndefu sana hatimaye tuliwasili nje ya hoteli kubwa na ya kisasa iitwayo Buffalo Hotel.
Ilikuwa ni hoteli nzuri mno!
Nakiri kuwa Tanzania na hata Afrika nzima hakuna nchi yenye hoteli nzuri kama ile ya Buffalo.
Tuliegesha gari letu eneo la maegesho kisha tulishuka na kuingia hotelini, ilikuwa ni hoteli ya ghorofa na Sam alitaka tupande ghorofa ya katikati hivyo tulikwea lifti iliyotufikisha moja kwa moja sehemu husika huko tulishuka na kutafuta sehemu inayotupendeza tukaketi, hatukuwa peke yetu walikuwepo na watu wengine wengi tu ambao tulikuwa pamoja kwenye mkutano walikuwa wakipata chakula.
<“Hapa unajihudumia mwenyewe!”\n “Haa wapi hapo?”
“Angalia wanakotoka watu na vyakula huko ndiko unaenda.”
Kweli nilivyotizama upande huo niliona wanakotokea watu na sahani za vyakula, haraka nilienda kwani na ushamba fulani ulikuwa ndani nilitamani sana nipaone huko wanakojipakulia chakula kupoje.
Nilifika!
Mmh!
Palipendeza lakini palitisha kwa upande mwingine.
Kwanza nikutana na mdada ambae ndiyo mtoa maelekezo pale, dada mwenyewe msafi halafu kajistili nguo mpaka nyayo hazionekani.
Baada ya salamu alinielekeza kuwa nachukua sahani (alinionesha mahali zilipo) kisha napita kwenye sufuria la chakula nipakue chakula kadiri ya ninavyojiskia halafu nipite kila sufuria nichovye kilichomo na kuchanganya kwenye chakula.
Sikutaka kupoteza muda nilienda kuchukua sahani nikaanza na sufuria la pilau nilikadiria chakula, kisha nikaanza mboga, sufuria la kwanza lilikuwa na nyama kavu za kukaangwa, nilitia vipande kadhaa, nikahamia sufuria la pili nikakutana na samaki walioungwa vyema nao nipo nilichota mchuzi kidogo na samaki mzima nikamtia kwenye chakula saa hiyo mate nayo yakileta usumbufu kinywaji sababu ya ulafi dhidi ya chakula kile kinukiacho harufu tamu.
Nikahami sufuria la tatu nikakuta mboga za majani hizo nilichota kidogo mno! Sikuwa nazitaka, nikaenda sufuria la nne!
Pale nilikutana na mchuzi wekundu, kama damu sikujua ni mchuzi wa aina ngani kwanza sikutaka kuusabahi sana sababu nilikuwa na hamu sana na chakula kile nilichokuwa nacho, nikachukua kijiko nikachota chuzi lile na kulitia kwenye pilau mara naona kidole cha mtu kinatumbukia humohumo.
Nilishtuka nikaganda kama sanamu, nikageuka nikamwangalia yule mhudumu nikaona nae ananiangalia.
Yaani isingekuwa ananiangalia sijui ningekifanyaje kile chakula maana hata hamu ya kukila iliyeyuka mithili ya kipande cha barafu jotoni.
Mara nikasikia Ko! Ko! Ko! Ko! Yule mhudumu anakuja mahali nilipo.
“Huyu mtu ana kwato au? Mbona zinalia Ko! Ko! Ko!?”
Nilijiuliza moyoni huku nikimtizama wakati akija.
“Vipi?”
Aliniuliza baada ya kufika.
“Hiki kiungo mimi hapana.”
“Sasa sheria yetu ukishachanganya chakula na mboga sharti ukile na si vinginevyo.”
“Nitalipia na hiki.”
“Walaa hatuna hiyo sheria.”
Nilishindwa kumwelewa mtu yule nikatamani hata kumporomoshea bonge la tusi sema nilimwogopa kwa kuwa simfahamu.
Niliondoka na sahani yangu nisijue nitaifanyaje sasa.

Nilifika mpaka nilipo mwacha Sam nilimkuta tayari yupo na Ledbull tatu na Don moja tayari keshaanza kujilipua.
Nilifika kinyonge na kuketi pembeni nikatulia kimya.
“Vipi umeleta nguna?… Halafu mbona umenuna?”
Aliongea kihuni kidogo.
“Hoteli gani sasa umenileta hii?”
“Kwanini?”
“Ona?”
Nilimwonesha kile kidole cha binadamu kwenye sahani ya pilau.
“Ooh!… Yess! Tamu sana hii kitu.”
Aliongea hivyo huku akikiokota kile kidole na kukitia mdomoni akaanza kukitafuna Kakachu…kakachu…kakachu hadi kilalainika akakimeza.
Nilibaki namtizma kwa macho yaliyojaa mshangao.
“Au lete hiki wewe nenda kapakue kingine huko ujiwekee mboga uitakayo.”
Aliongea huku akivuta kabisa ile sahani.
“Aah! Staki tena.”
Nilikataa nikavuta chupa la Don nikachukua Ledbull moja nikainywa hadi nusu kisha nikamimina Don ndani nikainywa ile pombe hadi ikaisha nayo niliinywa ovyoovyo.
“Sam mi nataka nirudi bwana.”
“Wapi duniani?”
“Ndiyo.”
“Si ndiyo urudi sasa?”
“Ningekuwa naweza ningeongea tena na wewe jamani kha!”
“Anhaa! Fanya hivi, kunja vidole viwili vya kati kisha vibabe na dole gumba halafu sinamisha vidole viwili cha mwisho na kile cha shahada halafu fanya kama unajinyoosha hivi.”
Nilifanya kama nilivyoelekezwa muda huohuo nikajikuta nipo najinyoosha kitandani pale Chek point.

Dah!
Ama kweli upande wa pili wa dunia kuna nguvu kubwa na ya ajabu sana.
Wakati ule nimetoka usingizini nilihisi haja ndogo imenibana ikabidi nijivilingishe shuka vizuri kisha nikaenda msalani nikamwaga maji na kurudi chumbani.
Nayo ikawa saa kumi na dakika arobaini jioni.
“Siku imeisha hapa niende wapi nikatulie halafu natakiwa kuipanga safari ya kwenda Dar maana siku zinakimbia mno.”
Niliongea kimoyo moyo huku nikiwa nimesimama pembeni ya kitanda, mara nikaona bahasha nyeupe ikiwa imeanguka chini, bila shaka niliiangusha wakati natoka kitandani.
Nikaokota, haikuwa na maandishi yoyote nje, hivyo niliifungua moja kwa moja ndani, huko nilikutana na picha na jina la mtu ‘Damson Mbalangu’ nilivyosoma tu jina nikakumbuka nini maana ya bahasha ile.
Haraka niliirudisha picha ile kwenye bahasha kisha bahasha nikaihifadhi kwenye mkoba wangu.
Niliingia bafuni nikajimwagia maji kuondoa jasho mwilini kisha nilirudi chumbani nikajipaka mafuta nikajipulizia na marashi kidogo kisha nilitoka tayari kichwani nilipanga niende Miami.
Nilipanga nitalala Miami kisha siku inayofuata nianze kufanya maandalizi kwaajili ya safari yangu ya kwenda Dar es salaam.
Nilipanga ninunue nguo nyingi na za gharama pamoja na begi kubwa la vigurudumu kisha kesho yake hiyohiyo nikate na tiketi kabisa ya kusafiria kesho kutwa yake.
Nilifika mwisho wa lami hapo nilichukua bodaboda iliyonikimbiza moja kwa moja mpaka Miami, nikashuka nikamlipa dereva bodaboda ujira wake akaondoka zake nami nikaanza kutembea kuelekea ndani.
Nayo ikiwa imetimia saa kumi na moja kamili alasili.
Hatua tatu za mwanzo nilizipiga pasi na shaka lakini nilivyopiga ya nne nikahisi kama kuna mtu ananifatilia nyuma yangu, nywele zilisisimka sana hata nikageuka kwa kasi nyuma, nikamwona yuleyule mwanaume rasta ambaye mwanzo nilimwona chek pointi pindi naenda kuchukua chumba cha kupumzika mchana ule.
Lakini ajabu licha ya kugeuka kwa kushitukiza nilimwona ndiyo kwaanza anaangalia pembeni mbali kabisa huku mkononi akiwa kashika simu janja.
“Mmh huyu mtu mbona namtilia shaka kiasi hiki?”
Nilijiuliza huku nikigeuka na kuanza kutembea mbele nikielekea ndani.
Nilipanda ghorofa ya juu huko nikatafuta sehemu tulivu nikakaa meza ya pekee yangu nikatulia.
Punde si punde mhudumu alifika kunisikiliza.
“Niletee savana tatu.”
Niliagiza.

Muda mfupi baadae vinywaji vilifika nikaanza kunywa taratibu, nilitoa simu yangu nikaanza kuperuzi, hata hivyo chaji ilishakuwa asilimia kumi bahati nzuri nilipoketi ukutani ilikuwepo soketi hivyo nilitoa chaja yangu kwenye mkoba nikachomeka kwenye soketi, ile nageuka nichomeke simu iliyokuwa mezani nilishitukia yule mwanaume anaketi taratibu kwenye kiti upande wa pili wa meza.
“Mambo vipi mrembo?”
Alinisalimia kwa kunichangamkia pindi anaketi kitini.
“Safi.”
Nilijibu kifupi.
“Naitwa Skobe… Samahani naweza kufahamu jina lako?”
“Naitwa Leylah.”
“Naam!… Jina zuri mno, vipii naweza jumuika nawe hapa au una mtu wako maalumu?”
Kufuatia swali lile nilimtizama kwanza usoni kwa kitambo kidogo, halafu nikavuta kumbukumbu kuhusu jina la Skobe.
Mmh!
“Aaa… hata kama atakuwepo we ukihitaji kujumuika katika meza hii ni ruksa.”
Mara mhudumu akafika kumsikiliza mteja mpya.
“Niletee value kubwa na glasi.”
Aliagiza.
Punde si punde nae alihudumiwa kisha kwa pamoja tulianza kunywa taratibu.
“Dada vipii mbona unakunywa vilaini?… Kwani vikali havikuchomoki?”
Aliuliza mwanaume huyo wakati huo akibwia pombe kali mfululizo.
“Kwa muda huu sijisikii kunywa pombe kali.”
Nilimjibu, ghafla ghorofa ya chini zilisikika purukushani kana kwamba kuna kamatakamata ya polisi imetokea.

Ghafla Skobe alitoa bastola na kuikamata mkononi, nikabaki nimeduwaa nisielewe nini kinaendelea, mara akasimama wima.
Hee nini tena na mimi nikasimama nikiwa mwenye hofu nyingi sana moyoni.
Mara polisi wawili waliingia kwa wakati mmoja chumba tulichokuwepo bunduki zikiwa imara mikononi mwao, palepale Skobe aliwafyatulia risasi mfululizo huku akiondoka mahali alipokuwa amesimama akasogea ukutani mahali lililopokuwepo dirisha la chumba kile kilichopo ghorofani.
Watu wote waliokuwamo humo ndani walilala chini sambamba na wale polisi waliovamia chumba, ni mimi tu ndiye sikukumbuka kulala chini.
Skobe aliendelea kufyatua risasi mfululizo ghafla alirukia dirishani akaning’inia nje.
“Anakimbia Samweli zunguka nyuma.”
Polisi mmoja kati ya wale wawili aliongea kwenye simu ya upepo huku akienda mbio pale dirishani.
Kitambo sana mabati yalishalalamika nje kuwa mwanamume huyo amekwishatua kwenye mapaa ya watu, muda huohuo mlio mkubwa wa pikipiki ulisikika nje pikipiki ikiondolewa kwa kasi ya kuogopeka.
“Sema sema Sam?… Ameshatembelea? Ooh shiit…”
Aliekuwa dirishani akiongea kwenye simu ya upepo huku akichungulia nje alilegea na kukosa nguvu baada ya kusikia msakwa kakimbia.
Basi wale polisi baada ya kuona wamemkosa msakwa wao waliondoka amani ikarejea.
Nayo ikawa yapata saa moja kasorobo jioni, bar ilianza kuchangamka watu waliendelea kuongezeka kama ilivyo kawaida ya baa zote nyakati za usiku.
Nami nililipia chumba cha kulala kabisa kabla ya kulala kisha nilirudi nikaendelea kunywa.
Baadae nilibanwa na haja ndogo ikanibidi nitoke niende msalani.
Sasa pindi nimeshajisaidia natoka mara niliona kivuli cha mtu kikinizunguka mgongoni, nilipotaka kugeuka nikahisi kuchuma cha baridi kimenigusa kisogoni.
Hurusiwi kugeuka wala kufanya chochote tulia hivyohivyo vinginevyo unapotea.
Nilitulia huku kitete kikinipanda kwa kasi ya aina yake.
“Vua huo mkoba.”
Niliamrishwa!
Sikuwa na namna nilianza kuuvua kwa papara.
“Taratibu taratibu!”
Aliongea kibabe huku akizidi kukandamiza kibomba cha bastola kisogoni mwangu, nikahisi mkojo usio na ratiba ukitoka na kuilowanisha nguo yangu ya ndani.
Lakini muda huohuo wazo la haraka lilipita kichwani nikawaza.
Simu yenye namba za akaunti yangu ya benki ipo kwenye mkoba! Maana niliitoa kwenye chaji nikaenda nayo chooni sasa pindi najisaidia niliiweka kwenye mkoba, haya mikataba yote ya mauziano ya nyumba ilikuwepo humo, bahasha yenye ranani ya kazi niliyopewa huko kuzimu ilikuwepo kwenye mkoba haya pesa zimo humo kiufupi huo mkoba ungenitoka umaskini nao ungechukua nafasi mara moja.
Ghafla nilihisi nguvu za ajabu zikiniingia mwilini, mbaya zaidi alichokuja kujikoroga akanifokea kwa sauti ya chini.
“Haraka wewe!”

Loh!
Palepale niligeuka na sambasoti moja ya aina yake! Hata hivyo aliiona akaikwepa kwa utaalamu wa hali ya juu! Ndipo akajibu pigo na judo moja mijarabu nayo niliiona nikamkatalia! Teke likapita hewani huku nikitoa na kimlusi fyuuuu!
Kitendo cha kulikwepa teke lile nilimshindilia na ngumi nzito ya sehemu za siri lakini kumbe ulikuwa ni mtego wake kwangu, kwani hakutetereka baadala yake nilijibiwa pigo na banzi moja takatifu hata nikahisi shavu linawaka moto, macho nayo yakaona maluwe luwe kibao.
“Mwiziiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiiii.”
Nilipiga ukunga wa nguvu baada ya kuona nimezidiwa.
Ghafla nikachomwa sindano ya paja palepale nikaona giza la ghafla machoni fahamu zote zikanipotea.

Sehemu 17 Sehemu 19
0
0