Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Dunia Ya Pili - 31

Kitendo cha gari kuzima ghafla kilinipa kihoro cha ghafla moyoni, wazo baya la kupigwa lilinijia kichwani.
“Nini?”
Nilihoji.
“Hata mimi sielewi.”
Alijibu sahiyo akishika funguo na kujaribu kuliwasha, alizungusha zungusha off kisha akazungusha on, stata ilikubali ila ililia tu mara mbili mishale yote ya dashboard ilipanda na kushuka kisha gari ikazima.
“Shiiiiit… Ni mafuta yameisha kwenye gari.”
Nilishusha pumzi kusikia hivyo, ilikuwa ni afadhali sana kuliko kuambiwa gari imeharibika.
“Sasa tunafanyaje?”
Nilimuuliza.
“Hapa inabidi nishuke nichukue boda maana sheli iko hapo mbele kidogo nifate mafuta.” Alijibu.
“Sawa.”
Nilikubaliana nae kisha nilimpa kiasi cha shilingi elfu sabini kwaajili ya mafuta.
“Hivi gari yetu inatumia mafuta gani?… Nisije nikanunua petroli kumbe inatumia dieseli.”
“Hapana inatumia dieseli.”
“Poa.”

Alishuka, akaondoka baadae alirudi akiwa na kiasi cha lita ishirini za mafuta, nilishuka nikahakikisha mafuta yawekwayo kwenye gari yangu, baada ya kujiridhisha mafuta yaliwekwa kisha dumu alipewa boda boda alirudishe sheli, si tukaingia garini Jr akawasha gari na kulitia moto tukaondoka zetu.
Baada ya mita kadhaa baada ya kuingia barabara kuu niliiona ile Crown ikiwa imeegeshwa mahali.
“Ile gari si ile pale we Jr?”
Nilimwonesha Jr.
“Kitambo sana nilishaiona achana nayo tuone tena kama watatufata.”
Alijibu saa hiyo akibadili gia na kufanya gari izidi kuwa nyepesi mno barabarani!
Mshale wa kusoma kasi za gari ulipanda kwa kasi mpaka kwenye namba 160 gari ilizidi kwenda kasi wakati huo dereva wangu akiwa makini sana na vioo vya pembeni yaani ‘Side mirror’ nafikiri umakini wake ulikuwa juu ya ile gari kama inaendelea kutufukuzia au la?!
Mpaka tunafika Kimara kona hakuna gari yoyote tuliyoweza kuishitukia kuwa inatufatilia nyuma, hapo Jr alihama barabara kuu akakatiza tukaingia vichochoroni huko tulitembea na barabara za vichochoroni, hata tukaja kutokea sehemu ilipo Bar iitwayo Kimara Kona nafikiri inaitwa hivyo sababu ya kuwa imejengwa mtaa uitwayo Kimara Kona.
Hapo tuliingia tukaegesha gari sehemu sahihi ya maegesho, ila kabla ya kushuka nilimtuliza Jr ndani ya gari kwa sababu nilikuwa na swali muhimu mno lililokuwa likitokota ndani ya mtima wangu.
“Eti Jr mi mbona sielewi eti?… Au wewe ndiye unaefuatiliwa?”
Nilimuuliza saa hiyo nikiwa na hamu kubwa na jibu lake!
Alicheka kidogo.
“Kwani awali kabisa aliefatiliwa na ile gari ni nani?”
“Toba!”
Nilishituka.
Kumbe anaefatiliwa ni mimi?
“Kuanzia kesho nitaanza kutembea na silaha ikiwa na risasi za kutosha pumbafu sitaki ujinga!”
Nilijisemea nafsini.

Mara nje mlinzi kaja na kilungu chake katugongea kioo.
“Ngo! Ngo! Ngo!… Oya hii siyo sehemu ya kuegesha gari na kuendelea kula kiyoyozi ndani.”
Aliongea mlinzi huyo akiwa nje ya gari.
Jr akashusha kioo.
“Vipi broo?”
“Safi… Vipi mbona mmeegesha gari halafu hamshuki?”
“Tunashuka kaka.”
“Poa, maana hii siyo sehemu ya kuegesha na kuendelea kula kiyoyozi kwenye gari bwana.”
Aliongea huku akiondoka zake mlinzi huyo!
“Ila njaa hizi duh.”
Alijiongelesha Jr saa hiyo akivuta hand breck ili gari isije ikajongea baadae.
Tulishuka moja kwa moja mijongeo yetu ikatia nanga kaunta kwa mara ya kwanza, hapo Jr aliongea mawili matatu na mhudumu wa kaunta kwa sababu muda huo alikuwa peke yake, akaagiza vinywaji pale kisha tukaondoka tukaenda kujichimbia kona moja tulivu tukiwa wawili tu.
Muda mfupi baadae vinywaji vililetwa zilikuwa chupa mbili kubwa za dompo na glasi mbili zikiwa na vitambaa safi vyeupe juu yake.
Mhudumu alitufungulia kabisa akatumiminia kwenye glasi kisha akaondoka zake.
Kimya cha muda mfupi kikakatiza katikati yetu.

Nilinyanyua glasi nikalainisha koo kwa funda mbili kisha nikaitua.
“Leylah!”
Niliitwa na Jr ilikuwa ghafla tu!
“Abee!”
Niliitikia saa hiyo nikiachia glasi pale mezani.
“Unajua nini?… Kuna kitu hukijui ambacho kiko nyuma yako! Ninaomba nikuambie.”
Moyo ukaluka taa!
“Niambie.”
Niliongea huku nikiwa na kihoro kikubwa sana moyoni.
“Damson Mbarangu ana kawaida ya kuteka waumini wageni na kuwaficha kisha anawaachia baadae iwapo ndugu zake watakuwa karibu halafu wakawaka!…
Na nje ya hapo ana kawaida ya kuteka watu kisha wanapotea kabisa!”

“Eeeh!”
Niling’aka! Nikaikumbuka bastola yangu!
“Ndiyo, unajua mimi ni mwenyeji ninaifahamu sana michezo yake iliyomingi, ndiyo maana nilivyoziona zile dalili tangu mwanzo niliamua kuchukua jukumu la kukulinda! Hata hivyo nimefurahi sana kupata kazi ambayo itafanya niwe nawe wakati wote maana itakuwa rahisi zaidi kukulinda.”
“Kwanini umeamua kuchukua jukumu hilo?”
Nilimuuliza huku nikimtizama usoni.
“Hata sijui ni kwanini?…Ila nimeona tu moyo unanisukuma kufanya hivyo.”
“Mmh!… Je, unafikiri unaweza kufanya hivyo na nisifanyiwe kile kilichopangwa juu yangu?”
Nilimuuliza swali la kimtego huku nikiwa makini sana na majibu yake isije kuwa naishi na mpelelezi nikaja kuingia kwenye mikono ya dola kirahisi kwa makosa ya mauaji ambayo kwangu yamekuwa ni kitu cha kawaida sana kutendwa na mikono yangu.
“Kwa sababu nakupenda, nipo tayari kupambana na chochote kitakachojitokeza mbele yako kukiwa na matokeo hasi juu yako.”
Nilicheka taratibu kisha nikanyanyua glasi nikanywa funda mbili kisha nikaitua mezani, ghafla mawazo yakamuwaza Damson Mbarangu.
“Damson Mbarangu unaonekana ni mtata siyo?… Lakini kwangu utaingia tu kwenye mfumo ikiwezekana hata penzi nitakumegea ili nikuue vizuri mshenzi wewe!”
Nilijiongelea nafsini huku nikichezesha vidole vya mkono wangu wa kulia.
Nikashtuka baada ya kutupa macho usoni pa Jr nikaona akiniangalia kwa udadisi mkubwa sana machoni.
“Mbona waniangalia sana Jr vipi?”
Nilizuga kumuuliza swali saa hiyo nikiokota glasi, niligundua ni kwanini Jr alikuwa akinitizama vile na sikutaka mada ile ikae mezani sababu nilijua yangekuja maswali mengi na yenye udadisi ambayo huenda katika majibizano huenda Jr angenitoa kwenye njia!
Sikutaka kuona hilo likitokea ndiyo maana nilianzisha mada mapema nikamwahi kwenye njia.
“Nakuangalia kwa sababu ni mzuri sana.”
“Haaaah!”
Nilijifanya kushituka kiaina saa hiyo moyoni nikijiuliza kumbe ndiyo unachowaza?
“Ndiyo ni mrembo sana ndiyo maana siishiwi hamu kukutizama usoni pako!”
“Toka uko! Halafu we jana usiku umenibaka wewe!”
“Hapana Leylah sijafanya hivyo kweli?”
“Ni kwanini uliniwekea dawa ya usingizi kwenye kinywaji kama hukuwa na hilo lengo na haukufanya hivyo?”
Nilimhoji kwa sauti kavu kidogo! Nae kusikia neno dawa ya usingizi akadata na kubaki kaganda kama mwanaume aliefumaniwa ugoni na mwanafunzi…!

Sehemu 30 Sehemu 32
0
0