Hello! Karibu HASCAVELA

Muonekano wa Giza:

Msaada

Dunia Ya Pili - 17

Hisia za kufuatiliwa na mtu zilinishawishi nitake kugeuka nyuma ili nione kama kuna mtu yeyote ningemtilia shaka lakini nilisita kugeuka nikaendelea kutembea mbele.
Nilifikia Check pointi bar kitendo cha kuingia na kuurudishia ule mlango wa kioo niligeuka kutizama nje wakati nikiwa ndani kutokana na uangavu mzuri wa mlango ule wa kioo kuna mwanaune mwenye rasta aliyevalia suruali ya jeans iliyomkaa vyema mwilini, juu akavalia t-shirt nyeupe yenye chapa ya kaa kifuani, miguuni alivalia buti safi la Amerika pamoja na saa kubwa ya mshare mkononi.
Nilimtizama ndani ya sekunde tano nikaona anakuja huku ndani bar.
Nikapotezea nikaenda zangu kaunta huko nikamuulizia mhudumu wa vyumba.
“Umemwacha kibarazani hapo nje kwani hujaona mdada mnene mnene hivi mweusi kavaa kimini cheusi na shati jeupe la mikono mirefu?”
“Nilimwona.”
“Ndiyo huyo, nenda uongee nae.”
“Sawa.”
Niligeuka nikatembea mpaka mlangoni nikaufunga ule mlango wa kioo nikatoka kibarazani huko nilimkuta huyo mdada anaongea na yule mwanaume nilietoka kumzungumzia muda mfupi uliopita.
Nilifikia hapo nikawasalimia kwa pamoja kisha nilimchukua yule dada pembeni nikamweleza shida yangu.
“Ahaa! Sawa ni shilingi elfu tano tu kupumzika.”
“Sawa twende unipeleke.”
Tuliingia upande wa vyumba huko akinionesha chumba kilichokuwa wazi, nikalipia nikaingia na kujifungia.

Wakati nikiwa chumbani kwangu simu yangu ilipigwa tena.
“Mmh nani tena huyu… Halafu usumbufu huwa sipendi mimi.”
Nilitoa kwenye mkoba na kuangalia kwenye kioo nilishituka kidogo baada ya kuona mpigaji ni Amina.
Nilianza kujishauri nipokee au niache iite hadi ikate kisha niizime.
Hata hivyo sikuona haja ya kufanya hivyo nilipokea tu ili nisikie ana shida gani.
“Hallo.”
Nilipokea.
“Waooo wifi yangu mimi.”
“Mambo!”
“Poa wifi mzima?”
“Mie mzima haswa hofu kwako.”
“Mie pia mzima… Sasa wifi yetu hata kuaga tu?”
“Ungejua vile nilichanganyikiwa hata sasa? Hata sijui nikuambiaje yaani Dah tuyaache tu.”
“Halafu muda mwingi kila nikipiga hupatikani, simu yako kila mmoja huku nyumbani analalamika tangu uondoke na simu imekuwa haipatikani hivi hata leo hapa nimekubahatisha tu, yaani nimesali kwanza kabla ya kukupigia naona Mungu amejibu maombi yangu.”
Nilishituka kwamba sipatikani.
“Sipatikani namna gani wakati simu yangu haijawahi kukosa chaji wala salio?”
Nilijiuliza bila kupata jibu.
Hata hivyo nilipotezea nikatafuta sababu ya kuongopa.
“Kweli bwana hata hapa nimeiwasha tu siyo muda sijiskii kutumia simu hata.”
Niliongopa wakati huo bado kichwani nikiendelea kutafakari ni kipi kinafanya nisipatikane kwa watu hao?
Nikajiuliza au huenda kuna siku nililewa nikawabrok?
Bado jibu kwangu halikupatikana.
“Jitahidi uwe hewani wifi yote kwa yote mimi bado nakupenda sana hata wenzangu pia, nyumbani wanahangaika sana kukutafuta kwenye simu hupatikani baba anaomba urudi basi urithi mali za mumeo, anasisitiza sana utulize akili uangalie maisha yako wifi.”
Amina aliongea vitu ambavyo kwangu viliingilia sikio la kulia na kutokea sikio la kushoto.
“Shangazi yupo? Nae nina muda sijaonana nae wala kuwasiliana nae.”
“Yupo lakini nae siku hizi katukasirikia hata salamu hatupi sijui ana nini nae moyoni kwake.”
“Mmh! Makubwa… Haya wifi nitakuja kuwasalimia.”
“Lini jamani wifi na nilivokukumbuka hivyo!”
“Hahahaha! Nitakujulisha usijali.”
“Poa wifi mchana mwema.”
“Sawa.”
Simu ilikatwa, nikaitupia pembeni kisha nikapunguza nguo nikajifunika shuka nikainza safari ya kuusaka usingizi.

Ilichukua muda kidogo kunichukua lakini hatimae ulianza kunijia nilianza kuhisi kope zinakuwa nzito hata nilipojaribu kuzifumbua kwa kulazimisha nilijikuta niko nje ya ngome kubwa ya shetani huko kuzimu huku mamia ya watu wakiendelea kumiminika kuja na kuingia ndani ya ngome hiyo.
Sikuwa naelewa chochote kuhusu ujio wa watu hao hata uwepo wangu pale, ikabidi nimsogelee mtu mmoja aliekuwa karibu.
“Habari ya saizi?”
Nilimsalimia, nilimsalimia kiswahili kwa sababu yule alionekana ni mtanzania kabisa tena Mzanzibari.
“Safi zako kwako?”
“Njema… Eti samahani mbona naona watu wanakuja kwa wingi wanaingia humo ndani kuna nini?”
“Kwani haukuwa na taarifa?”
“Mimi ni mgeni.”
“Mwenyeji wako yuko wapi?”
Maswali yake yalinikera nikajikuta namkasirikia nikaachana nae nikaanza kuondoka zangu.
“Sasa unakwenda wapi?”
Akauliza.
“Sasa wewe nakuuliza nawe unaniuliza maswali sasa ningefanyaje?”
“OK nilitaka kujua kuhusu wewe ila kama unakasirika kuulizwa sawa, ila leo kuna mkutano mkubwa wa Lucifer hapa nafikiri hata wewe ujio wako ni kwaajili ya huu mkutano hivyo ongozana nami tungie ndani kuuhudhuria.”
Basi tukaingia ndani kwa pamoja na yule mtu.
Watu walishafurika mule ndani kama nyuki, wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee, baadhi ya watu wenye vyeo vikubwa sana duniani mfano baadhi ya wachungaji wenye makanisa makubwa na waanzilishi wa baadhi ya makanisa, maparoko, masista, mabraza na wainjilist wengi sana walikuwepo katika mkutano huo achilia mbali wanamuziki kuanzia wa nchi yetu hata nchi za nje asilimia kubwa walihudhuria mkutano ule, wacheza filamu wakubwa, watangazaji wa vituo mbalimbali vya habari duniani, wamiliki wa makampuni, viongozi wa nchini mbalimbali duniani, viongozi wa vilabu mbalimbali vya mipira duniani hata wachezaji, madereva , marubani, manahodha na kadhalika walikuwepo.
Ulikuwa ni mkutano mkubwa sana.

Nusu saa baadae mkutano ulifunguliwa, agenda zikaweka bayana mazungumzo yakaanza.
Lucifer tayari alikuwepo kwenye kiti chake kirefu cha dhahabu kilichotengenezwa mfano wa kinu.
Agenda kuu ilikuwa kuhusu mpango wa pombe maalumu iliyopangwa kutengenezwa na kuchanganywa na sumu kwaajili ya lengo fulani.
Lucifer aliuliza mpango huo unakwendaje? Ikiwa ni takribani siku kadhaa zimepita tangu mpango huo ujadiliwe.
Papo hapo alisimima mwanaume mmoja alianza kujitambulisha jina kisha akajitambulisha na cheo chake alijitambulisha kuwa yeye ni mkurugenzi katika kampuni fulani jina tutalihifadhi, kampuni inayojihusisha na utengenezaji pamoja na kusambaza pombe fulani pendwa sana.
Mkurugenzi huyo alikuja na jibu kwa Lucifer, alijibu kuwa mpango huo unakwenda vizuri sana kwani tayari kampuni hiyo imekwishauanzisha mpango wa kutengeneza toleo la pili la pombe ileile na mpaka kufikia wakati huo tayari mpango huo ulikuwa umefikia asilimia sitini na akaahidi kuwa kufikia mwezi unaofata pombe hiyo itakuwa tayari na itaanza kusambazwa huku kukiwa na ofa kabambe kwa watumiaji.
Watu wote wakapiga makofi.
Lucifer akaja na agenda nyingine, safari hii alikuja na agenda ya mpira, alisema kuwa mwaka ujao kungekuwa na mashindano ya kombe la dunia na yeye binafsi angependa kombe hilo safari hii liende Australia.
Ndipo rais wa nchi hiyo aliposimama na kutolea maelezo kuhusu takwa la Lucifer.
Kiongozi huyo alisema kuwa yeye angetoa kiasi cha lita elfu kumi za damu kama shukran kwa Lucifer kwa kumheshimisha katika mashindano hayo ya kandanda ya kombe la dumia mwaka unaofuata.
Watu wakapiga makofi.
Lucifer akaja na agenda nyingine tena kwa wachezaji, viongozi wa vilabu mbalimbali duniani, agenda ililenga wao kuchukua makombe ya ligi, makombe ya shirikisho na makombe ya bara, tuzo za uchezaji bora, tuzo za kocha bora, tuzo za timu na kadhalika.
Kila kiongozi wa timu, na mchezaji alijidhatiti kwa maelezo pamoja na ahadi ya kafara kwa Lucifer ili kufanikisha malengo yao kimpira.
Mkutano uliendelea.
Lucifer alikuja kwa madereva, akauliza je wanataka usalama wao barabarani, kuepukana na ajali zisizo za lazima? Kudumu kazini? Kupendwa kazini? Na kupata kazi haraka pindi wakosapo kazi?
Jibu kwa kila dereva lilikuwa ni ndiyo, nae akawapangia kila mmoja kuleta damu ya nduguye ili kufanikisha hilo.
Akaja kwa viongozi wa makampumi akawaponda kidogo, kwa kuwaambia kuwa wengi kampuni zao zimeshuka sana kifedha na kibiashara sababu wamekuwa wakijisahau sana kwenye suala la sadaka akawahimiza kuwa sadaka ni muhimu sana katika kuimarisha kampuni na mifumo yote ya kiundeshaji.
Akaja kwa viongozi wa makanisa mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali duniani, aliwahimiza kuhakikisha hawaendi tofauti na mpango wao, aliwaasa kutosahau majukumu yao ili mafanikio yawe kwao.
Akawaomba pia wasijisahau sana kwenye upande wa sadaka hasa kipindi cha mwisho cha mwaka.
Katika jambo la kushangaza kuna kiongozi mmoja mkubwa sana wa kanisa fulani hapa nchini alisimama kitini na kutoa heshima zake kwa Lucifer kisha alisema yeye kupitia kauli ya nchi za magharibi anataka kuhalalisha ndoa za jinsia moja katika kanisa lake.
Watu wote waliokuwamo mule ndani walipiga makofi mengi sana.
Lucifer akampongeza na akasema nguvu kubwa kutoka kuzimu itakuwa karibu nae mbele ya nyuso za watu kuhusu uamuzi wake, lakini akawaonya viongozi hao wa kidini kutomuasi hapo baadae kwani yeyote ambaye angethubu kumsaliti basi jeshi lake lingempoteza katika uso wa dunia haraka sana.
Kikao hiki kilichodumu zaidi ya masaa matatu kilimalizika ambapo baadae kila mmoja alipita mbele ya Lucifer akaongea nae mawili matatu kisha alipewa bahasha na kuondoka, baadae zamu yangu ilifika.
Nilienda huku nikiwa natetemeka mwili mzima kwa hofu ya kuonana ana kwa ana na kiumbe huyu atishae kwa mara ya kwanza naenda kuongea nae ana kwa ana nikiwa najua kuwa ni shetani.
Nilifika kwenye kiti chake kikubwa cha dhahabu kilichojengwa juu ya madhabahu ya mawe ndani ya ngome yake.
“Leylah, nakupa bahasha hii nikiwa natambua kuwa una safari ya kwenda Dar es salaam…
Nenda uwapo Dar es salaam utakutana na sifa za mchungaji fulani anaitwa Damson Mbalangu hakikisha pindi uwapo Dar es salaam fanya kila liwezekanalo umwondoe duniani kwa sababu ametuasi sisi na sasa hivi anajifanya kueneza neno la mungu.”

Aliongea hivyo tu kisha akaniruhusu kwa ishara niondoke.
Dah niliondoka na bahasha yangu mkononi huku nikihisi hata miguu imekuwa mizito kutembea.

Sehemu 16 Sehemu 18
0
0